Watumishi wa Serikali ya Tanzania wadaiwa kutolipa madeni NHC

Tuesday October 22 2019

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Baadhi ya watumishi wa Serikali ya Tanzania wametajwa kutolipa madeni wanayodaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Hayo yameelezwa leo Jumanne Oktoba 22, 2019 na mkurugenzi wa shirika hilo, Sophia Kongole.

Sophia alieleza hayo wakati akijibu maswali ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mjini Dodoma.

Amesema shirika licha ya kupitia kipindi kigumu limejitahidi kukusanya madeni kwa asilimia 80, kubainisha kuwa madeni sugu watumishi hao ni kikwazo.

Shirika hilo liliitwa mbele ya kamati hiyo kutoa maelezo kwa nini limekuwa likificha taarifa zake na kukabiliwa madeni makubwa.

Sophia amesema bado wanakabiliwa na mambo mengi kutokana na mfumo walioukuta.

Advertisement

Amebainisha kuwa pamoja na kukusanya madeni uendeshaji wa shirika umefumuliwa kwa ajili ya kujipanga upya na kwamba wamesitisha huduma ya kuuza nyumba kama ilivyokuwa awali. Amesema kwa sasa wanakodisha.

“Tumeyumba lakini shirika halitakufa. Tuna madeni tunayopambana nayo, na tuna mkakati tuliojiwekea tangu tumeanza kazi. Naomba kamati yako itusamehe mwenyekiti (wa kamati) tutabadilika,” amesema Sophia.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly  amesema hali ya shirika hilo ni mbaya na inatishia shirika hilo kufa kwa kuwa kuna anguko la asilimia 50.

Aeshi amesema tangu Novemba 2016 PAC imekuwa ikiomba taarifa sahihi za shirika hilo lakini hawapewi, “ imekuwa danadana kiasi cha kutufanya kuamini kuwa ndani yake kuna madudu.”

Makamu mwenyekiti huyo alikataa taarifa ya shirika hilo kwa maelezo kuwa inatakiwa kupitia kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kutaka ipelekwe huko kabla ya kuwasilishwa tena kwenye kamati hiyo Novemba 24, 2019.

Advertisement