VIDEO: Watumishi watano wa TRC wafa kwenye ajali ya treni

Muktasari:

Watumishi watano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wamefariki dunia baada ya treni ya uokoaji kugongana na kiberenge jana Jumapili 22, 2020 katika maeneo kati ya stesheni za Mwakinyumbi na Gendagenda.

Dar es Salaam. Watumishi watano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wamefariki dunia baada ya treni ya uokoaji kugongana na kiberenge.


Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumatatu Machi 23, 2020 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Masanja Kadogosa amesema watumishi hao wamefariki dunia jana Jumapili maeneo katikati ya stesheni za Mwakinyumbi na Gendagenda.


Tarifa iliyotolewa na shirika hilo na kuthibitishwa na Kadogosa imesema kuwa ajali hiyo iliyotokea iliua watumishi wanne papohapo na kujeruhi wawili.
“Ni kweli hiyo taarifa inayozunguka kwenye mitandao tumeitoa sisi na watumishi watano wamefariki kwenye ajali hiyo,” amesema Kadogosa akizungumza na Mwananchi
“Watumishi wa TRC walikuwa sita, watumishi wanne wamefariki pale pale katika eneo la ajali na majeruhi wawili walifikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya (Magunga) Korogwe kwa huduma za kitabibu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.


Majeruhi mmoja alifariki dunia akiwa hospitalini akipatiwa matibabu na kufikisha vifo vitano.
Taarifa hiyo imewataja waliofariki dunia kuwa ni; Ramadhani Gumbo, Fabiola Moshi, Joseph Komba, Philip Kajuna na George Urio.


Kuhusu maandalizi ya mazishi ya watumishi hao shirika limesema litatoa taarifa likisema uchunguzi utafanywa kubaini chanzo cha ajali hiyo.