Wawili wakamatwa na madawa ya binadamu, vifaa tiba vya MSD bila kibali

Boksi lenye madawa ya binadamu na vifaa tiba alivyokutwa navyo mtu mmoja anayedai kuwa ni daktari katika hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro ambavyo mali ya Serikali. Picha Hamida Shariff

Morogoro. Jeshi la polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na madawa mbalimbali ya kutibu binadamu pamoja na vifaa tiba vyenye nembo ya MSD kwenye gari lake aina ya Harrier bila ya kuwa na kibali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Aprili 1, 2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Willbroad Mutafungwa amemtaja mtuhumiwa wa kwanza kuwa ni Barnabas Mayunga ambaye alikamatwa Machi 21 mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi katika maeneo ya Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro akiwa na madawa na vifaa tiba hivyo mali ya Serikali.
Kamanda Mutafungwa amesema baada ya mtuhumiwa huyo kuhojiwa alidai kuwa yeye ni daktari hata hivyo taarifa za awali zinadai kuwa mtuhumiwa huyo miaka ya nyuma aliwahi kuwa mtoa huduma za afya katika hospitali hiyo ya rufaa hata hivyo polisi bado wana mashaka na taaluma ya mtuhumiwa huyo na hivyo wanaendelea na uchunguzi zaidi.
“Bado tuna mashaka na taaluma yake ya udaktari anayodai kuwa nayo, tumeona twende mbali zaidi kwa kufuatilia vyeti yake, shule na vyuo alivyosoma na kufuatilia namna alivyoajiriwa kwa fani hiyo ya udaktari,” amesema Kamanda Mutafungwa.
Kamanda Mutafungwa amemtaja mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa na madawa ya binadamu pamoja na vifaa tiba kuwa ni Daniel Nelson mkazi wa Wilaya ya Gairo na kwamba awali mtuhumiwa huyo alikamatwa kwa tuhuma za kumtorosha binti kutoka kwa wazazi wake na baada ya kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa na madawa na vifaa tiba hiyo bila ya kuwa na kibali.
Amesema pamoja na kutuhumiwa kumiliki dawa kinyume cha sheria lakini pia mtuhumiwa huyo ambaye awali alikuwa akifanya kazi kwenye zahanati ya misheni Gairo anadaiwa kutoa huduma za matibabu nyumbani kwake kwa njia ya kificho na bila ya kufuata utaratibu, hata hivyo bado polisi wanaendelea kumuhoji.
Vifaa hivyo ni pamoja na dripu sita, dawa za sindano, gloves, maji ya kuchanganyia dawa za sindano, mabomba ya sindano, mashine ya kupimia BP, paracetamol boksi moja, amoxline 7, sare ya kijani moja, vitabu vitano vya matibabu ya wagonjwa, fomu za matibabu 4 na mikasi.