Waziri Bashungwa aahidi ndani ya siku 30 kukifufua kiwanda cha Chai Iringa

Monday January 20 2020

Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent

Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa akikagua mashamba ya chai yaliyotelekezwa na wakulima wa kidabaga wilayani Kilolo kwa kukosa kiwanda cha kupeleka kuuza chai. 

By Berdina Majinge,Mwananchi [email protected]

Kilolo. Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa amesema atahakikisha ndani ya mwezi mmoja kiwanda cha chai Kidabaga kilichopo Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kinaanza kufanya kazi ili kuinua kipato cha wakazi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.

Bashungwa ametoa ahadi hiyo leo Jumatatu Januari 20,2020 wakati akitembelea kiwanda cha chai Kidabaga kilichopo Wilaya ya Kilolo na kusema matumaini ya wana Kilolo ya kupambana na umasikini yanategemea kiwanda cha chai.

Amesema moja ya maelekezo ambayo Raisi wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza ni kuhakikisha wanakiondoa kiwanda hicho kwenye historia yakuwa godauni na kuwa kiwanda kinacho zalisha chai.

"Nitahakikisha ndani ya mwezi mmoja maeneo yote serikalini yanayokwamisha kiwanda cha chai kufanya kazi kila mmoja atachukua wajibu wake ili kifanye kazi. Lengo ni kutaka wakulima wa chai waendelee kulima chai na kiwahakikishie kiwanda hiki kinafufuka kwa sababu tayari tunaye mwekezaji," amesema Bashungwa

Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah amesema wananchi wamekuwa na kilio cha kufufua kiwanda cha chai kwa sababu wanayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha wanachangia pato la taifa.

“Imekuwa ni kilio cha muda mrefu takribani miaka 20 kiwanda hiki hakijafanya kazi lakini bado jitihada zinaendelea za kuhakikisha kinafufuliwa na kuanza kufanya kazi na wakulima msikate tamaa ya kulima chai," amesema Asia

Advertisement

Mbunge wa Kilolo (CCM) Venance Mwamoto amesema Serikali tayari imejipanga kutengeneza barabara za mashambani hadi kiwandani kuhakikisha kiwanda kinapoanza kazi barabara inakuwa nzuri kwa ajili ya usafirishaji.

"Chai baada ya kuvunwa haitakiwi kukaa muda mrefu barabarani hivyo serikali tayari imeandaa bajeti ya barabara ya Kidabaga ili kurahisisha usafirishaji wa zao hilo," amesema

Joseph Mwamsungu mkazi wa Kijiji cha Kibadaga amesema kusimama kwa kiwanda hicho kimesababisha vijana wengi kukosa ajira na uchumi wa kidabaga kuwa chini kutokana na watu wengi kulima miti ambayo inachukua miaka 20 kuvunwa tofauti na chai huchukua miaka mitatu.

 

"Kufufuka kwa kiwanda hiki kitatusaidia sisi vijana kuwa na mashamba mengi ya chai ambayo faida yake hupatikana baada ya miaka mitatu, tofauti na mashamba ya miti na kwa kupitia kiwanda hiki vijana watapata ajira," amesema Mwamsungu

Advertisement