Waziri Jafo aibuka tena, akana kauli yake

Muktasari:

Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania utakaofanyika Novemba 24, 2019 umekuwa ukimuibua Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo na kutoa kauli tofauti na leo ametoa nyingine akikana ile aliyoitoa jana Jumapili.

Dodoma. Suala la uchaguzi wserikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 unaendelea kumuibua Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo katika sura tofauti.

Leo Jumatatu Novemba 11, 2019 Waziri Jafo amezungumzia uchaguzi katika kauli mbili tofauti na sasa ameelekeza kuwa, watakaoingia kwenye uchaguzi ni walioteuliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi pekee.

Kwa kauli hiyo, ni dhahiri kuwa, amerudisha mamlaka kwa wasimamizi ambao jana Jumapili alikuwa amewapoka jambo lililozua mjadala mkubwa kwa wadau.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jioni Jumatatu katika ofisi za wizara hiyo zilizoko Mtumba jijini Dodoma, Waziri Jafo amesema kauli yake ya jana Jumapili ilikuwa imenukuliwa vibaya.

"Kumekuwepo na tafsiri na uelewa tofauti wa maelezo niliyoyatoa jana Novemba 10, 2019 kuhusu wagombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24,2019," amesema Jafo.

Waziri amesema wagombea watakaokuwa na haki ya kugombea ni waliopitishwa na kuteuliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi pekee na siyo vinginevyo.

"Waombaji wote ambao walichukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi za uongozi na kisha wakateuliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi," amesema.

Waziri ametaja wengine ni waombaji wote waliowasilisha pingamizi kwa wasimamizi  wa uchaguzi kuomba kuteuliwa na pingamizi zao zikakubaliwa pamoja na waombaji waliokata rufaa kwenye kamati za rufaa za wilaya na rufaa zao kukubaliwa.

Amewaagiza wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri zote nchini kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo  kikamilifu.

Mapema leo asubuhi akijibu mwongozo wa mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftah Nachuma, Waziri Jafo alisema kauli yake ya jana itasimama hivyo hivyo.

"Mheshimiwa Spika, jana nilitoa kauli kuhusu wagombea wanaotakiwa kuingia kwenye uchaguzi na kwa siku ya leo no more comment," alisema Jafo akiashiria kauli yake ya jana ilikuwa ndiyo ya mwisho.

Mchango wa wabunge leo kwa sehemu kubwa umejikita kwenye uchaguzi huo kwa wabunge wa upinzani kulalamika na wabunge wa CCM wakionyesha kuunga mkono kuwa uchaguzi uko sahihi.