Waziri Jafo atakiwa kuingilia kati mahusiano ya RC Iringa na madiwani

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Grace Tendega akichangia mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) nchini Tanzania, Grace Tendegu amesema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi amekuwa na mahusiano mabaya na madiwani mkoani humo na hivyo kuwakatisha tamaa.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Grace Tendega amemuomba Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo kushughulikia tatizo la mahusiano mabaya ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi na madiwani wa mkoani humo.
Grace alikuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Grace amesema lipo tatizo la viongozi wakuu wa mikoa wanawadharau madiwani.
Amesema alikwenda Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutokana na mahusiano mabaya aliyonayo mkuu huyo wa mkoa wengi wa madiwani walitaka kugoma kwenda.
“Mkuu wa mkoa akienda kwenye kata hasalimii madiwani. Madiwani wamekuwa ni wanyonge hadi hawana hamu na kufanya kazi na mkuu wa mkoa. Amekuwa akiwadhalilisha kuna madiwani wawili kata za Ulanga na Masaka aliwaweka ndani,”amesema.
Amemuomba Jafo kuangalia jambo hilo kwasababu wanawakatisha tamaa madiwani na kwamba hao ndio wanaowatafutia kura wabunge na Rais.
“Viongozi wanapaswa kuwa na hekima katika nchi. Ni vyema ifike mahali viongozi kuheshima,”amesema.
Kuhusu stahiki za madiwani, Grace amesema madiwani hawalipwi stahiki zao ipasavyo na kutoa mfano wa Wilaya ya Biharamulo ambapo madiwani wamekatwa fedha zao kwa ajili ya kulipia mikopo lakini hazikupelekwa,” amesema.
Hali kadhalika, Gace amemtaka Jafo kutamka bungeni kuwa ni shilingi ngapi zilitengwa kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.
“Maeneo yaliyomengi uchaguzi haukufanyika. Karibia asilimia 90 hayakufanya uchaguzi kwasababu wagombea walipita bila kupingwa. Tunaoomba chenji yetu irudi iende kwenye afya kwenye barabara,”amesema.