Waziri Jafo atoa ujumbe mwingine kwa wapinzani kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa

Muktasari:

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijini na Vitongoji nchini Tanzania utafanyika Novemba 24, 2019 huku baadhi ya vyama vya upinzani vikiwa vimetangaza kutoshiriki uchaguzi huyo kwa madai ya kutokutendewa haki. Vyama hivyo ni Chadema, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi pamoja na Chaumma.

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo amesema hakuna kuhamisha goli tena zaidi ya kauli yake ya jana Jumapili kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Jafo ameliambia Bunge leo Jumatatu Novemba 11,2019 wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftah Nachuma ambaye alitaka Bunge litoe dakika 30 ili wabunge wajadili kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mafutah aliomba mwongozo huo baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni lakini akasema kitendo cha Waziri Jafo kuruhusu uchaguzi uendelee hakisaidii kitu kwani tatizo ni watu kutopewa nafasi ya kurudisha au hata kuchukua fomu kabisa

Jana Jumapili, Waziri Jafo alitangaza wagombea wote waliochukua fomu na kuzirudisha waruhusiwe kuingia kwenye uchaguzi ili wananchi wakaamue wenye.

Hata hivyo, kilio kikubwa cha wapinzani ni kuwa maeneo mengi wapinzani ama walizuiwa kuchukua fomu au walizuiwa kurudisha fomu zao kwa watendaji kufunga ofisi au kuzifungua kisha kuondoka na kuziacha wazi.

"Mheshimiwa Spika kama kuna watu wanapaswa kumuogopa Mungu basi wawe ni hawa, jana nilisema lakini leo wanataka kuhamisha goli sasa spika nasema no more comment katika hili," amesema Jafo na kukaa chini huku akipigwa makofi na wabunge wa CCM na kufanya wapinzani wengi kusimama ingawa hawakupewa nafasi.

Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wapinzani kuingia kwenye mchakato kama alivyowapa nafasi hiyo Waziri Jafo ambaye alisema hakuna kuweka mpira kwapani.

Katika mchango wake, mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM) Ali Keisy amesema wapinzani hawana hoja na kuwa wamebaki wachache kwani kazi za Rais John Mahufuli ni nzuri huku akimkaribisha mbunge wa Iringa Mchungaji (Chadema), Peter Msigwa kurudi CCM.