Waziri Jafo azungumzia uchaguzi serikali za mitaa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleimani Jaffo

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleimani Jaffo amesema tarehe ya uchaguzi wa serikali za mitaa itatangazwa muda wowote kuanzia sasa huku kampeni zikipangwa kufanyika siku saba kabla ya uchaguzi.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inatarajiwa kutangazwa tarehe maalum ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa huku kampeni za uchaguzi huo zikifanyika kwa siku saba kabla ya siku ya uchaguzi.

Pia, uandikishwaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo utafanyika siku 47 kabla ya uchaguzi.

Hayo yalisemwa jana Jumatatu Agosti 19,2019 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleimani Jaffo katika mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha Azam.

Alisema kutakuwa na tukio rasmi la kutangaza tarehe ya uchaguzi ambayo pia itaenda sambamba na ugawaji wa kanuni zitakazosimamia uchaguzi.

“Hakuna mtu anayejua tarehe ya uchaguzi, japokuwa vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa vilishiriki katika uandaaji wa kanuni, katibu tawala, asasi za kiraia, wakuu wa wilaya na mikoa,” alisema Waziri Jafo

Akizungumzia kujiandikisha alisema licha ya kufanyika kwa uchaguzi kama huo mwaka 2014 na watu kujiandikisha lakini hawatakuwa na sifa ya kupiga kura mwaka 2019.

“Kutakuwa na daftari jipya, kila kanuni inakuja na daftari lake, watu watajiandikisha katika mitaa yao na itakuwa ni siku 47 kabla ya.”

“Na kabla ya uchaguzi, kutakuwa na siku saba za kampeni na kwa serikali za mitaa ni nyingi sana kwa sababu siku moja wanaweza kumaliza mitaa yote na kwa hizo siku tulizotoa si ajabu wakapita nyumba kwa nyumba,” alisema Jaffo.