Waziri Kalemani ataja maeneo yenye ‘harufu’ ya mafuta Tanzania

Wednesday October 2 2019

Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Merdard

Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Merdard Kalemani 

By Kelvin Matandiko Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Merdard Kalemani ametaja maeneo manne yanayoashiria matumaini ya ugunduzi wa rasilimali ya Mafuta nchini kwa siku za usoni kupitia shughuli za utafiti zinazoendelea.

Maeneo aliyoyataja ni pamoja na ya ukanda wa Ziwa Rukwa, Ziwa Tanganyika na Kitalu cha Eyasi Wembere chenye ukubwa wa kilometa za mraba 19. 2.

Kitalu hicho kinapita katika mikoa ya Arusha, Manyara, Simiyu, Shinyanga na Tabora.

Dk Kalemali ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 2, 2019 Jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Mafuta na Gesi.

 

“Kuanzia eneo la Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa, maeneo ya Pwani ya Tanga pamoja na Kitalu cha Eyasi Wembere, tunashukuru timu ya wataalamu ya Uganda inayosaidiana na Shirika letu la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kusaidia ushauri,” amesema Waziri Kalemani.

Advertisement

Tathmini ya Idara ya Mkondo wa Juu wa TPDC ilibaini matumaini makubwa ya ugunduzi wa rasilimali hiyo yanapatikana zaidi katika maeneo yaliyopitiwa na Bonde la Ufa na ukanda wa Pwani.

Imeelezwa kuwa matumaini ya Tanzania kugundua rasilimali hiyo yanachagizwa na jiolojia ya maeneo yaliyo kwenye bonde la ufa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushabihiana, ikiwamo Uganda iliyogundua mafuta katika Ziwa Albertine huku Kenya ikigundua katika eneo la Lokichar.

 Katika ufafanuzi wake, Waziri huyo  amezitaka kampuni zote za kimataifa zilizoshiriki katika kongamano hilo pamoja na zile zinazomiliki mikataba ya ugawanaji mapato (PSA) kupanua mtandao wa uwekezaji Tanzania, kwa kuwa mfumo wa sera na mazingira ya uwekezaji ni rafiki.

Waziri Dk Kalemani amesema kauli mbiu ya Serikali ya Tanzania kwa sasa imejikita katika maeneo ya kuhamasisha na kuwezesha ukuaji wa sekta binafsi, kuchochea matumizi ya bidhaa za ndani, kuimarisha mazingira ya uwekezaji pamoja na kuchochea ukuaji wa viwanda.

Advertisement