Breaking News

Waziri Mkuchika awaonya viongozi wanaokaa na barua za uhamisho

Friday December 6 2019

By Nazael Mkiramweni, Mwananchi [email protected]

Dodoma.  Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti, Utumishi wa Umma na Utawala Bora nchini Tanzania, Kepteni mstaafu George Mkuchika amewakemea viongozi wa umma wanaokaa na barua za uhamisho wa watumishi bila kuwafikishia wahusika.

Mkuchika ameyasema hayo jijini Dodoma leo Ijumaa Disemba 6, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu yatakayofanyika Desemba 11, 2019 jijini Dodoma.

Amesema kuna watu baadhi ya viongozi wanachukua nafasi ya Katibu Mkuu Utumishi kwa kukaa na barua za wafanyakazi wao kinyume cha sheria za utumishi wa umma.

 

"Ndani ya Serikali wapo viongozi wamekuwa na tabia ya kukaa na barua za uhamisho wa watumishi, unakuta mtu kaandika barua ya kuomba kuhamishwa lakini barua hiyo inapojibiwa viongozi wao wakiipokea hawaikabidhi kwa mhusika, wanakaa nayo."

"Huu si utumishi bora kwani kiongozi huyo anaifanya wizara kuonekana imechelewa kujibu barua hiyo na wizara inajua kuwa tayari mtumishi huyo kahamishwa, niwaambie kuwa kama mtumishi huyo bado unamuhitaji toa hoja za msingi ili asiondoke lakini si kukaa na barua yake," amesema Mkuchika

Advertisement

Amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo wanapanga kufanya semina kwa viongozi na watumishi wa umma kuhusu utawala bora na misingi ya maadili.

Advertisement