Waziri Mkuu azindua wiki ya vijana kitaifa Lindi

Waziri Mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji katika ngazi zote kuhakikisha vijana wanawezeshwa kushiriki shughuli za maendeleo.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji katika ngazi zote kuhakikisha vijana wanawezeshwa kushiriki shughuli za maendeleo.

Amesema tayari Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ikiwa ni pamoja na maeneo ya ujenzi wa viwanda vinavyomilikiwa na vijana.

Ametoa agizo hilo leo Alhamisi Oktoba 10, 2019 wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa mwaka 2019 kwenye viwanja vya Mpilipili nje kidogo ya mji wa Lindi.

“Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo hadi mwishoni mwa mwaka 2018 zaidi ya ekari 217,882.36 zilikwishatengwa. Ninaziomba Halmashauri zote zisimamie na kutekeleza agizo hilo ili kuhakikisha maeneo hayo yanatumiwa kama ilivyokusudiwa.”

“Vijana  tushirikiane na Serikali kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo. Hatua hii itatuwezesha kama Taifa tuvuke na tufikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” amesema mAJALIWA.

Ametembelea mabanda mbalimbali ikiwemo banda la kikundi cha vijana kutoka China, Korea Kusini, Argentina, Arzebhaijan na Tanzania ambao waliishi kwenye mazingira magumu na wakabadilika na wameamua kushiriki maonesho hayo ili kuwabadilisha mtazamo vijana wenzao.

“Nimefurahi kuwaona hawa vijana, ninaamini watashirikiana na wenzao wa hapa kuwabadilisha vijana wa Tanzania ili wawe na fikra endelevu,” amesema.

Akizungumzia mikakati ya kuwawezesha vijana kiuchumi, Majaliwa amesema ofisi ya waziri mkuu imeanza kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba katika Mikoa yote na Halmashauri zote nchini.

Amesema teknolojia hiyo itawasaidia wakulima kupata mazao mengi kwenye eneo dogo na kupata mazao bora yanayokidhi viwango katika soko la ndani na nje ya nchi.

“Kwa kutumia teknolojia hii, vijana wengi watapata ajira katika sekta ya kilimo,” amesema.

Amebainisha kuwa mkakati huo ni utekelezaji wa agizo la CCM, chama kinachotambua kuwa sekta ya kilimo ndio kimbilio la wananchi walio wengi na kupitia ilani yake ya mwaka 2015 Ibara ya 6 (a) inayoeleza; kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao.

Kabla ya kumkaribisha Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amesema sambamba na kuboresha sera ya elimu na mafunzo, Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa programu ya kukuza ujuzi nchini iliyolenga kutoa mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi kwa vijana.

“Mpaka sasa vijana 32,736 wameshapata mafunzo na mwaka huu ofisi ya waziri mkuu vijana wengine 46,000 watapata mafunzo mbalimbali ikiwemo kilimo cha kisasa,” amesema.