Waziri Mpango aelezea mikakati ya kuiboresha TRA

Wabunge na Mawaziri wakisoma kitabu cha hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, ilipokuwa ikiwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipinga, Dk Philip Mpango, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameelezea mikakati mbalimbali itakayotumika katika mwaka wa fedha 2019/20 ya ukusanyaji mapato na kushughulikia kero za malalamiko dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewasilisha Makadirio na Mapato kwa mwaka 2019/20 ikiwa imependekeza hatua mbalimbali za kuchukua za kisera na utawala katika kuimarisha na kurahisisha ukusanyaji mapato.

Akiwasilisha makadirio hayo leo Alhamisi Juni 13, 2019 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema ili kuondoa malalamiko ya wafanyabiashara dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imeamua kuanzisha kitengo huru cha kupokea malalamiko na taarifa za kodi ambacho kitaratibiwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Amesema kitengo hicho kitahusisha kupokea na kupitia malalamiko ya taarifa za Kodi zitakazotolewa na walipakodi au watu wenye nia njema. Baadhi ya majukumu ya Kitengo hicho ni kama yafuatayo:-

 

  1. Kupokea malalamiko ya rushwa dhidi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania;

 

  1. Kupokea malalamiko ya ukadiriaji wa Kodi na uthaminishaji wa bidhaa usio wa haki wala uhalisia dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania;
  2. Kupokea malalamiko ya matumizi ya nguvu katika ukusanyaji kodi dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania;

 

  1. Kupokea malalamiko ya ufungaji wa biashara bila kufuata sheria na taratibu dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania; na

 

  1. Kupokea malalamiko pamoja na kero nyingine zinazofanana na hayo dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
  1. Ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya kodi za ndani, serikali inakamilisha manunuzi ya mfumo unganishi wa kielektroniki (Intergrated Domestic Revenue Adminstration System- IDRAS) katika kukusanya kodi na mapato yasiyo ya kodi ili kuleta uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Pia mfumo huu utarahisisha ulipaji wa kodi na kupunguza rushwa miongoni mwa watumishi wasio waaminifu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania;
  2. Kuendelea kusimamia matumizi ya  mfumo wa kukusanyia kodi wa kielektroniki (Electronic Fiscal Device Management System) ambao umefanyiwa maboresho makubwa na kuanza kazi tangu tarehe 1 June, 2019, ili kudhibiti na kubaini udanganyifu unaofanywa katika matumizi ya mfumo huo. Aidha, hatua hii itadhibiti uvujaji wa mapato katika urejeshaji wa kodi ( Tax refund), utoaji wa risiti bandia, n.k;
  3. Kutokana na wimbi la vijana wengi kujihusisha na michezo ya kubahatisha na kusahau majukumu ya ujenzi wa taifa, Serikali ikishirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha imebuni na kutengeneza mfumo maalum ambao utatumika kudhibiti uchezaji wa michezo hii (Responsible Gaming). Pia, Mfumo huu  utatumika kudhibiti udanganyifu ambao unafanywa na waendeshaji wa michezo ya kubahatisha ili Serikali ipate mapato yake halali;
  4. Kutokana na malalamiko ya walipa kodi kuhusu ukadiriaji wa kodi na uthaminishaji wa bidhaa usio na haki wala uhalisia, Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuanzisha dawati la kushughulikia mapingamizi ya makadirio ya kodi ambapo pingamizi za uthamanishaji na utambuzi litashughulikiwa ndani ya masaa ishirini na nne (24); na
  5. Kutoa unafuu wa kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita (6) kuanzia wakati mfanyabiashara au mwekezaji anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN). Hatua hii inatofautiana na hali ilivyo sasa ambapo mfanyabiashara anapopewa TIN anaanza kufanyiwa tathmini (tax assessment) ya mapato yake ya biashara na kutakiwa kulipa kodi. Hatua hii itawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wapya kupata muda wa kujiandaa na mahitaji yanayotakiwa katika shughuli wanazofanya na kuondoa usumbufu au dhana ya woga wakati wa kuanzisha biashara. Mfano kuna mahitaji ya Leseni ya biashara na vibali vingine muhimu.