Waziri Mpango awapongeza wafanyakazi wa wizara yake

Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Philip Mpango

Muktasari:

Serikali imeridhishwa na utendaji kazi wa wafanyakazi wake wanaokwenda kwenye masomo Uingereza kwa fursa zinazotolewa na Shirika la DFID kwa lengo la kuiwezesha Serikali kuboresha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma na kuongeza mapato ya ndani.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Philip Mpango ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa wafanyakazi katika wizara yake ambao walipata nafasi za masomo Uingereza kwa udhamini wa Serikali ya nchi hiyo.

Dk Mpango ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 19,20190 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwatunuku tuzo wafanyakazi wa wizara hiyo ambao wanatarajia kwenda kusoma Uingereza Septemba 2019.

Mpango huo unaosimamiwa na British Council Tanzania na kufadhiliwa na Shirika la misaada la DFID, ulianzishwa mwaka 2017 kwa lengo kuisaidia Serikali ya Tanzania kusimamia fedha, kuboresha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma na kuongeza mapato ya ndani.

“Ninafurahi kuona utendaji kazi wa wafanyakazi wetu waliopitia hii programu unaridhisha. Kwa niaba ya serikali, ninapenda kutoa shukrani za dhati kwa serikali ya Uingereza kupitia shirika la DFID kwa mchango huu muhimu. Program hii imeongeza thamani ya rasilimali watu ya serikali,” amesema Dk Mpango.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la DFID nchini, Beth Arthy amesema programu hiyo ambayo imetimiza miaka mitatu sasa ni ushahidi wa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Uingereza.

Baada ya kukamilika kwa masomo yao, wafanyakazi hao wa wizara wanatarajiwa kurudi kufanya kazi kwenye wizara hiyo kwa kuleta mabadiliko sambamba na kutekeleza sera ya viwanda na kuisaidia serikali kupunguza umasikini na kukuza uchumi.