Waziri Mwakyembe kushawishi wabunge wa Tanzania wavae vitenge, batiki

Muktasari:

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema atawasilisha ombi kwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ili atoe kibali kwa wabunge kuvaa mavazi ya asili bungeni kama batiki na vitenge

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Dk Harrison Mwakyembe amesema bunge lijalo atamwandikia barua Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ili atoe kibali kwa wabunge  kuvaa batiki na vitenge wanapokuwa bungeni.

Pia, anatarajia kupeleka barua katika ofisi ya Tamisemi ili maofisa wa utamaduni nchini waruhusiwe kuvaa mavazi hayo.

Dk Mwakyembe amezungumza hayo alipokuwa akifungua maonyesho ya sanaa ya mavazi na ubunifu Swahili Fashion Week yaliyoanza jana Ijumaa Desemba  6 hadi kesho Jumapili Desemba 8, 2019.

Alisema atapendekeza nguo hizo ziwe za ziada kwa wabunge wawapo Bungeni  badala ya kung'ang'ania vazi la suti pekee.

Dk Mwakyembe amesema Bunge la Tanzania lijalo atamuandikia barua Spika huyo awaruhusu wabunge kuvaa vitenge au batiki wanapokuwa bungeni kama itashindikana amruhusu waziri huyo kila Ijumaa awe anavaa nguo hizo.

Alifafanua  akiruhusiwa atawavutia wabunge wengi hivyo na wao watakuwa mstari wa mbele kuomba kuvaa mavazi hayo ambayo yatawapendeza na itaongeza uchumi kwa vijana wabunifu wa mavazi hayo.

"Kuna maombi maalumu ya wabunifu wa mavazi wameomba kwa Spika wa Bunge watuonyeshe nguo gani nadhifu mbunge anatakiwa kuvaa halafu na sisi tutapendekeza bungeni nguo ya ziada ya mbunge kuliko kung'ang'ania tai zinatubana wakati mwingine.

“Sisi ni Waswahili tunatakiwa tuwe huru tujivunie vya kwetu, sawa tuvae tai, suti lakini vya kwetu je vitenge, kanga na batiki kwa nini tusivae," alihoji Dk Mwakyembe.

Pia, aliwataka Watanzania kuangalia ubunifu wa ndani iwe namna ya kuongeza thamani kwa bidhaa zinazozalishwa mfano wakina mama wengi wanatengeneza nguo za batiki, vitenge na kanga ni njia pekee ya kuongeza thamani kwa kushona.

Dk Mwakyembe alitolea mfano wa wizara yake. kila Ijumaa wanavaa vitenge na batiki ambayo ni mishono ya ubunifu.

Naye Mwalimu wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta Dar es Salaam, Athanasia Kisyeli alisema anatamani wahudumu wa ndege nao wavae mavazi yanayowatambulisha ni Watanzania.

Kisyeli alisema “Bila ya kusema mavazi yanasema yenyewe kwa rangi ya Tanzania inaonyesha madini, ngozi na rasilimali zake hivyo ukizivaa huwezi kuulizwa umetokea nchi gani.”