Waziri Ummy atangaza siku tano za chanjo ya rubella

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto nchini Tanzania, Ummy Mwalimu

Muktasari:

  • Watoto chini ya miaka 5 katika halmashauri zote nchini wanatarajia kupatiwa chanjo ya rubella na surua katika kampeni maalumu iliyoandaliwa na wizara ya afya.
  • Rubella ni ugonjwa ambao dalili zake huendana na zile za surua na hupimwa kwa watoto ambao tayari wameathiriwa na surua ndiyo maana chanjo zake hutolewa kwa wakati mmoja.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto nchini Tanzania, Ummy Mwalimu ametangaza wiki moja kwa ajili ya kutoa chanjo ya rubella na surua kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano katika halmashauri zote nchini humo.

Chanjo hiyo itaanza kutolewa kati ya Septemba 25 hadi 30, 2019.

Waziri huyo ameyasema hayo leo Jumatatu Septemba 9, 2019 jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi magari 71 yaliyo na thamani ya Sh7.7 bilioni.

Magari hayo yamenunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambao ni Shirika la The Global Alliance for Vaccines and Immunisation (GAVI Alliance) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) kwa ajili ya kuimarisha usambazaji wa chanjo ambapo 61 kati yake yameelekezwa katika halmashauri.

Amesema lengo la kutoa chanjo hizo ni kutaka kuhakikisha magonjwa hayo yanakomeshwa huku akihamasisha watu wengi zaidi kushiriki.

“Takwimu zinaonyesha kuwa dola 1 ya kimarekani itakayowekezwa katika chanjo inaokoa dola 6 za kimarekani zinazoweza kutumika katika matibabu hivyo ni vyema tukaweka nguvu nyingi katika upande huo.

“Tunaomba wakina mama ambao wana watoto hawa kujitokeza kwa wingi kuwapeleka katika vituo vya kutolea chanjo ili kuwakinga magonjwa lakini pia tutatumia fursa hiyo kutoa chanjo ya kupooza,” amesema Ummy

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka wizara ya afya,  Leonard Subi amesema licha ya kutolewa kwa magari hayo katika halmashauri lakini bado yanahitajika zaidi ili kurahisisha ufikishaji wa chanjo katika sehemu husika.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau wetu ili kuhakikisha chanjo hizi zinawafikia walengwa ndani ya wakati muafaka,” amesema Subi