Waziri Zungu kuanza na mifuko ya plastiki

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu amesema licha ya Tanzania kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, siku za hivi karibuni imeanza kurejea sokoni.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu amesema licha ya Tanzania kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, siku za hivi karibuni imeanza kurejea sokoni.

Zungu ambaye ni mbunge wa Ilala (CCM) ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 27, 2020 muda mfupi baada ya kula kiapo Ikulu, Dar es Salaam.

Zungu ameteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira kuchukua nafasi ya George Simbachawene aliyehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya uteuzi wa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola kutenguliwa.

Zungu amesema wizara aliyopewa ni ngumu na ina changamoto nyingi, kubainisha kuwa katika suala hilo Baraza la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) linapaswa kujiuliza maswali.

“Watu wa Nemc tuulize kwa nini vitu hivi bado vipo nchini, kwa nini vitu hivi bado vinapita katika mipaka, viko mitaani na havina nembo ya biashara au ya mtengenezaji kama kanuni inavyosema.”

“Mheshimiwa Magufuli nakuahidi hili nitalifanyia kazi kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kwa vizazi vya sasa, kesho na vya baadaye,” amesema Zungu.

Waziri huyo amesema atatoa ushirikiano kwa wafanyakazi wa wizara hiyo huku akiwataka wawekezaji waliotimiza masharti ya vibali waonane na mamlaka husika ili kuepusha kuzuia uwekezaji hasa wa viwanda.

Mbali na Zungu na Simbachawene, pia mabalozi walioteuliwa na Rais Magufuli wameapishwa leo.