Waziri akagua ukarabati reli Arusha-Moshi, atumia saa tatu njiani

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe akishuka kwenye Kiberenge katika Stesheni ya Arusha wakati akikagua njia hiyo kutoka mkoani Kilimanjaro leo. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ametumia saa tatu kusafiri kwa kutumia Kiberenge cha Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutoka mjini Moshi hadi Arusha umbali wa kilometa 72.

Arusha. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ametumia saa tatu kusafiri kwa kutumia Kiberenge cha Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutoka mjini Moshi hadi Arusha umbali wa kilometa 72.

Akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko leo Alhamisi  Februari 27,2020, Kamwelwe ameeleza kuridhishwa na kasi ya ukarabati wa reli unaoendelea kati ya eneo hilo.

"Tumetoka Moshi saa 3:30 asubuhi niwapongeze mafundi wetu wa TRC na vibarua wanaoshirikiana nao kuhakikisha tunatekeleza  maagizo ya Rais John Magufuli kufufua kila kilichokufa katika awamu zilizopita," amesema Kakoko.

Kadogosa amesema ukarabati huo ulikwamishwa na uharibifu wa reli mkoani Tanga, “tulilazimika kuwapeleka mafundi huko kwanza kuweka mambo sawa.”