Waziri ashangazwa wananchi Ukerewe kulipishwa umeme mara 25 ya wengine

Waziri wa Nishati, Dk Medadi Kalemani akijibu maswali bungeni katika kikao cha pili cha mkutano wa 18 wa Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dk Medard Kalemani ametoa maagizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhakikisha anafuatilia gharama za umeme zinazotokwa kwa wananchi wa kisiwa cha Ukerewe mkoani humo.

Dodoma. Watumiaji wa umeme katika Wilaya ya Ukerewe Mkoa wa Mwanza nchini Tanzania wanatumia nishati hiyo kwa gharama ya Sh2,500  kwa uniti moja badala ya Sh100 inayotozwa kwa maeneo mengine.

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Januari 29, 2020 na Mbunge wa Ukerewe (CCM), Joseph Mkundi wakati akiuliza swali la nyongeza akiitaka Serikali ya Tanzania kuchukua hatua.

Mkundi amesema kwa hali hiyo, mwananchi wa Ukerewe anatumia gharama hiyo mara 25 ya mwananchi mwingine wa maeneo nje ya Ukerewe hali ambayo ni tofauti kubwa.

Akijibu swali la nyongeza la mbunge huyo, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema jambo hilo halikubariki.

Dk Kalemani amesema Mtanzania yeyote anayetumia umeme usiozidi uniti 70 kwa mwezi, anapaswa kulipia kiwango cha Sh100 kwa uniti siyo gharama ya huko.

"Hali hiyo haikubariki tena ni uonevu, namuagiza mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa waingilie kati jambo hilo na wananchi  wasikubari kuuziwa umeme wa gharama hizo," ameagiza Dk Kalemani.

Kuhusu  kukatika kwa umeme, Dk Kalemani amesema chanzo ni  wavuvi wamekuwa wakikata nyanya.