Waziri asimamishwa kazi kwa kukiuka amri ya kutotoka nje

Muktasari:

Ni waziri wa Habari wa Afrika Kusini ambaye alienda kupata chakula cha mchana na rafiki yake.

Johannesburg, Afrika Kusini. Waziri wa Habari wa Afrika Kusini amesimamishwa kazi kwa miezi miwili baada ya kukaidi amri ya kutotoka nje.

Wananchi wa Afrika Kusini kwa sasa wanatekeleza amri ya kutotoka nje iliyotolewa na Rais Cyril Ramaphosa kwa lengo la kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

 Stella Ndabeni-Abrahams, alipewa adhabu hiyo ambako mwezi mmoja atakaa nyumbani bila kulipwa mshahara.

Waziri huyo amezua gumzo tangu picha yake iliyomuonyesha akila chakula na rafiki yake aliyetambulika kwa jina la Mduduzi Manana kusambaa mitandaoni.

Picha hiyo iliwaonyesha marafiki hao wakifurahia chakula pamoja na wanafamilia wa Manana ilichapishwa kwenye moja kati ya akaunti za mitandao ya kijamii nchini humo.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Aprili 8 na Rais Ramaphosa ilisema kuwa hajashawishika na sababu zilizotolewa na waziri huyo baada ya mazungumzo yao.

“Hakuna miongoni mwetu atakayepuuza juhudi zetu za kuokoa maisha wakati huu. Hakuna aliye juu ya sheria,” alisema Rais Ramaphosa.

Mara baada ya uamuzi huo, waziri huyo aliomba radhi wananchi wa Afrika Kusini kwa kitendo hicho.

“Nasikitishwa na kitendo change, ninatumai Rais na raia wa Afrika Kusini watanisamehe,” aliongeza

Awali rafiki wa waziri huyo ambaye ni naibu waziri wa zamani, alisema alimtembelea kwa sababu za kikazi.

Alisema alikwenda nyumbani kwake ili kuchukua barakoa ambazo alikuwa anataka kuzitoa kupitia taasisi yake kusaidia mapambano dhidi ya corona.