Waziri mkuu asema hospitali ya kanda itarahisisha huduma

Muktasari:

Kukamilika kwa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini kutarahisisha zaidi ya wananchi 4.5 milioni kutoka Lindi, Mtwara na Ruvuma  na wa nchi jirani ya Msumbiji kupata huduma za afya  na hivyo wananchi kutakiwa kutojihusisha na wizi wa malighafi.


Mtwara. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mradi wa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini Mtwara, itawarahisishia wananchi wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kupata huduma kwa karibu badala ya kwenda Dar es Salaam.

Mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu Sh15.8 bilioni  na kuhudumia zaidi ya  watu 4.5 milioni, tayari mkandarasi ameshakabidhiwa Sh6.2 bilioni.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 2, 2019 alipokuwa akizungumza na wananchi alipotembelea Mitengo kuona maendeleo ya shughuli za ujenzi na kumtaka mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuzingatia muda.

“Hospitali hii ni muhimu  na imewekwa hapa kimkakati, ni muhimu kwa watu wa kusini hatuna tena sababu ya kwenda Dar es Salaam, tuliamua kuiweka Mtwara ili sisi (Lindi) tuje hapa kwa ufupi na watu wa Ruvuma, na Rais John Magufuli ameshapiga lami mpaka Songea hawana safari ndefu sasa wanapita hapa (Mtwara) kwenda Dar es Salaam,” amesema Majaliwa.

Kutokana na ujenzi huo, amewataka wenyeji wa mikoa hiyo kuwapa ushirikiano NHC ili kuhakikisha wanakamilisha mradi huo katika mazingira rahisi kwa kuzingatia suala la ulinzi kwa manufaa ya wote.

“Iko tabia ya maeneo yote ya ujenzi hasa wa kiserikali watu wanadhani mali ya serikali ni mali ambayo unawezakuichukua tu, kwa hiyo hatutarajii kupata tatizo la wizi hapa kuja kuiba nondo, saruji, mabomba au kuiba nyaya za umeme,” amesema Majaliwa na kuongeza;

“Kwa kufanya hilo tunajikamisha wenyewe, ni muhimu sana madiwani kusema kwa wananchi eneo hili waliache na anayeingia hapa ni yule aliyeridhiwa kuingia na sio wale wa kuja kuiba vifaa..nilipata aibu sanana uchungu sana nilipokwenda mji wa Moshi  tunawajengea kituo cha mabasi cha kimataifa siku ile ile wakaiba nondo tani tano,” amesema Majaliwa.

Mkurugenzi Mkuu  wa NHC, Dk Maulid Banyani amesema mradi huo unatakiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja na kuahidi endapo hawatakumbana na kikwazo chochote watapunguza miezi mitatu ya mkataba na kukamilika kabla ya Agusti 31,2020 kama ilivyo katika mkataba.

“Tayari Serikali imeshatupatia Sh6.322 bilioni hizi tutazitumia mpaka tufike mahala tutaweza kuonyesha jengo limesimama, mkataba ambao shirika la nyumba limeingia na Wizara ya Afya, mradi unatarajiwa kukamilika Agosti 31, 2020 ahadi yetu tunatarajia tutafanya kazi usiku na mchana na pale tutakapokuwa hatuna kikwazo chochote tutapunguza miezi mitatu kwenye mkataba,” amesema Dk Banyani

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza mwaka 2005 hadi kufikia 2015 tayari ilikuwa umeshatumia Sh 2.7 bilionilakini serikali ya sasa imeweza kutenga 15.8 bilioni ndani ya mwaka mmoja.