Waziri wa Fedha wa Tanzania ataja changamoto za bajeti kwa mwaka 2018/19

Muktasari:

Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dk Philip Mpango ametaja changamoto zilizoikabili bajeti ya mwaka 2018/19 ikiwamo ukwepaji wa kodi kwa njia mbalimbali.

Dk Mpango ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 5, 2019 wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21 bungeni.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mahitaji makubwa yasiyowiana na uwezo wa mapato na ukwepaji kodi kwa njia mbalimbali na  kutokutoa stakabadhi za kielektroniki na kuendesha biashara za magendo hususan kupitia bandari bubu maeneo ya mipakani.

Changamoto nyingine ni mabadiliko ya viwango vya riba katika masoko ya fedha ya nje, kutopatikana kwa misaada na mikopo kutokana na baadhi ya washirika kutotimiza ahadi zao kwa wakati na ukosefu wa takwimu za uwekezaji wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Dk Mpango amesema katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa bajeti, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwianisha mapato na matumizi.

 

“Kuimarisha ulipaji wa kodi wa hiari kwa kutekeleza Mpango wa kusimamia vihatarishi vya mwitikio wa ulipaji kodi, kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi ya mashine za stakabadhi za kielektroniki kupitia matumizi ya mfumo ulioboreshwa, kuongeza doria na ukaguzi unaolenga kudhibiti biashara za magendo,” amesema.

Nyingine ni  kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji, kukuza soko la fedha la ndani,  kuendeleza majadiliano na washirika wa maendeleo na taasisi za fedha za nje, kutekeleza mwongozo wa ushirikiano baina ya Serikali na washirika wa Maendeleo.

Dk Mpango amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kupata taarifa za uwekezaji wa sekta hiyo katika uchumi.