Waziri wa zamani amvaa Zitto mkopo wa Benki ya Dunia, Spika Ndugai amshangaa

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendoi), Zitto Kabwe

Muktasari:

Sakata la mkopo wa elimu kutoka Benki ya Dunia (WB) limetinga  bungeni baada Waziri wa Zamani wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Joseph Kakunda kueleza kusikitishwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo) Zitto Kabwe kuandika barua ya kuzuia fedha hizo katika benki hiyo.

Dodoma/Dar. Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Joseph Kakunda amesema kitendo cha Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendoi), Zitto Kabwe kuandika barua ya kutaka kuzuia mkopo wa elimu unaotolewa na Benki ya Dunia (WB) ni kituko nani aibu.

Kakunda ameyasema hayo jana Alhamisi Januari 30, 2020 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia taarifa za kamati za Bunge za bajeti na Uwekezaji na Mitaji ya Umma.

Mkopo huo wa masharti nafuu ni wa Dola milioni 500.

 “Naomba nizungumze masikitiko yangu dhidi ya barua moja ambayo mwenzetu mmoja (Zitto) ameiandika kutaka kuzuia fedha za miradi ya elimu ni kituko na ni aibu sana kwetu sisi wabunge kuona mwenzetu ameandika barua,” alisema Kakunda ambaye pia ni Mbunge wa Sikonge (CCM) mkoani Tabora

Alisema barua hiyo wangekuwa wameandika watu wa mashirika yasiyo ya kiserikali yeye asingestuka sana lakini kuandikwa na mbunge mwenzao wakati Serikali imepeleka Sh1 bilioni kwa ajili ya kukarabati Sekondari ya Kigoma iliyoko kwenye jimbo lake ni jambo la kusikitisha.

“Sasa hivi Sekondari ya Kigoma ni kama mpya. Na vilevile Serikali imepeleka zaidi ya Sh4 bilioni kwa ajili ya kuboresha elimu. Sasa anazuia zisije kwa haraka kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kitanzania nieleze masikitiko makubwa sana,”amesema.

Alitaka kutumia elimu kuwasaidia watoto wa Kitanzania badala ya kuwacheleweshea maendeleo kwa kuzuia shule 1000 na wanafunzi 600,000 kunufaika na fedha hizo za Benki ya Dunia.

“Nilitamani nipaze sauti huko aliko anisikie lakini kwa sababu yuko mbali naachia hapo lakini atasikia kutoka kwenye Hansard (kumbukumbu Rasmi za Bunge).

Leo Ijumaa Januari 31, 2020 bungeni jijini Dodoma, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wanamsubiri Zitto awaeleze kwa nini aliandika barua hiyo.

“Mtu unaweza kuwa na tofauti na sera au mtazamo kati ya wewe mbunge au upande wa Serikali na kadhalika, lakini kufikia mahali pa ‘kublock’ Tanzania isipate fursa fulani nadhani ni kwenda mbali mno.”

“Kwa sababu watoto watakaokosa fursa hiyo ni watoto wa Tanzania ni walimu wa Tanzania ni miundombinu ya elimu ya Tanzania, sijui katika hilo kama mbunge unanufaika nini maana kama ni suala la utofauti la kisera haya ni mambo ya kujadiliana tu,” amesema Spika Ndugai.

Katika kusisitiza hilo, Spika Ndugai amesema, “ningependa kutoa ushauri wa ujumla tu kwamba ni vema kutumia fursa yetu kama wawakilishi wa wananchi tukaelimishana tukaelezana kuliko kuwakosesha Watanzania fursa wakati baadhi yetu watoto wetu wapo Feza Boys, wapo Marian Girls halafu unablock msaada kwa watoto walio wengi wa wapiga kura wetu jambo ambalo halifai kabisa.”