Wenye magonjwa haya wachukue tahadhari zaidi dhidi ya corona

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amewashauri watu wenye magonjwa mbalimbali kuchukua tahadhari zaidi katika kukabiliana na ugonjwa wa corona ambao hadi sasa maambukizi yake nchini yamefika kwa watu 32 na kupoteza maisha ya watu watatu.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter, Dk Ndugulile amesema kuwa mtu mwenye magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu, pumu, ugonjwa wa moyo na unene uliopitiliza huathirika zaidi na Covid-19.
Dk Ndugulile ameongeza kuwa mtu mwenye magonjwa hayo yupo kwenye hatari zaidi na anaweza kupoteza maisha.
Ameshauri watu kuchukua tahadhari zaidi kwa kupima afya na kuzingatia ushauri wa kitaalamu juu ya magonjwa hayo ili kupunguza madhara zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, Aprili 10, 2020 jumla ya watu walioambukizwa ugonjwa wa corona imefika 32, na waliofariki dunia kwa ugonjwa huo ni watu watatu.