Wizara ya Afya yataja sababu gharama vipimo Muhimbili kuwa juu

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustin Ndugulile akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Wizara ya Afya nchini Tanzania imesema wagonjwa wanaokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) bila kufuata taratibu za rufaa ndio chanzo cha kuongezeka kwa gharama za vipimo

Dodoma. Wizara ya Afya nchini Tanzania imesema wagonjwa wanaokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) bila kufuata taratibu za rufaa ndio chanzo cha kuongezeka kwa gharama za vipimo.

Hayo yameelezwa na naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa Septemba 13, 2019, kubainisha kuwa utaratibu wa kupata huduma katika hospitali lazima ufuatwe

Katika swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Kisangi amehoji kwa nini wananchi wanatozwa gharama kubwa mara mbili wanapokwenda kuomba huduma za vipimo.

Katika swali la msingi mbunge huyo ametaka kujua Serikali ina mkakati gani kupeleka mashine za kufulia katika hospitali za Rufaa Amana, Mwananyamala na Temeke ambazo hazina mashine hizo.

"Wagonjwa wote ambao wanapitia taratibu za rufaa kuanzia ngazi ya zahanati huwa wanahudumiwa vipimo hivyo kwa gharama ndogo lakini mgonjwa ambaye hajapitia hatua hizo hutozwa gharama kubwa kwani anahesabika kama mgonjwa binafsi," amesema Dk Ndugulile

Kuhusu mashine katika hospitali hizo,  amesema taratibu za kununua mashine zinaendelea kwani Amana imeshatenga eneo kwa ajili kujenga chumba cha utakatishaji huku wakiwa kwenye mchakato wa kununua mashine kubwa ya Sh80 milioni.

Amesema Temeke wameshaagiza mashine yenye uwezo wa kufua kilo 70 kwa awamu moja na pasi yake kwa Sh83.34 milioni na Mwananyamala wameagiza mashine mbili za Sh71 milioni na tayari moja imeshapelekwa katika Hospitali hiyo.