Zantel kinara usajili laini za simu, TTCL hali ngumu

Dar es Salaam. Wakati siku 17 zikiwa zimesalia kabla ya kumalizika kwa muda kusajili laini za simu kwa alama za vidole, kuna uwezekano watumiaji wa mtandao wa Zantel wakakamilisha kazi hiyo kabla ya muda huo ambao ni Desemba 31.

Zantel imebakiza wateja wenye laini 573,891 tu ambao hawajajisajili.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano (TTCL) liko nyuma katika usajili, ikiwa imesajili laini 215,917 pekee kati ya laini zake zote milioni 1.04.

Ripoti ya hali ya usajili wa laini kwa alama za vidole iliyotolewa jana na TCRA inaonyesha kwamba mtandao wa Zantel pekee ndiyo umeweza kusajili angalau nusu ya watumiaji wake.

Usajili huo umekabiliwa na tatizo la wananchi kutokuwa vitambulisho vya Taifa, nyaraka muhimu katika usajili huo. Ili uweze kusajili laini ya simu kwa alama za vidole ni lazima uwe na kitambulisho hicho ambacho kinatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Mkurugenzi mkuu wa TCRA, James Kilaba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kuna laini milioni 47.064 ambazo zinamilikiwa na watu milioni 21.2 katika mitandao tofauti.

Wateja wa mitandao ya Vodacom, Tigo, Airtel, Smile na Halotel bado wako nyuma katika kusajili laini zao, wakati usajili ukitarajiwa kuhitimishwa Desemba 31.

“Tunasisitiza kwamba watu wajitokeze kwenda kusajili laini zao kwa kutumia namba za kitambulisho cha Taifa, hata kama bado hujakipata,” alisema akizungumzia wale ambao wameanza mchakato wa kufuatilia vitambulisho na kupewa namba wakati wakisubiri nyaraka hiyo muhimu.

“Kuna kundi kubwa la watu ambao namba zao za kitambulisho ziko tayari, lakini hawajasajili laini zao na pengine hawajui kama ziko tayari.

“Huhitaji kwenda Nida ili kupata namba yako ya kitambulisho, unaweza ukatumiwa kupitia simu yako na ukasajili laini yako.”

Mkurugenzi wa mambo ya kisekta wa TCRA, Dk Emmanuel Mannaseh alisema laini ambazo wamiliki wake wana namba za utambulisho za Nida lakini hazijasajiliwa kwa njia ya alama za vidole ni milioni 5.6 ambazo zinamilikiwa na takribani watu milioni tatu.

Alisema mwongozo wa watumiaji wa huduma za mawasdiliano umeweka utaratibu wa kusajili laini zinazotumiwa na watu binafsi, kampuni au taasisi, watoto, raia wa kigeni, maofisa wa ubalozi na wanadiplomasia.

Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni za simu kwenye mkutano huo, William Mpinga alisema usajili bado unakwenda taratibu, hivyo ni jukumu la kila mdau kuhakikisha kwamba suala hilo linakwenda haraka.

“Siyo tu kwamba mapato ya kampuni za simu yatapungua, bali pia wananchi watapata usumbufu wa kupanga foleni wakati wa kufanya malipo,” alisema Mpinga.

Naye mkurugenzi mkuu wa Nida, Dk Anold Kihaule amewataka wananchi kwenda kujisajili kupata kitambulisho cha Taifa kama njia ya awali ya kusajili laini kwa alama za vidole.