Zanu-PF yamtaja Mugabe shujaa wa Taifa

Sunday September 8 2019

 

Harare.  Chama tawala cha Zimbabwe, Zanu-PF kimemtangaza Rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe aliyefariki dunia Ijumaa kuwa ni shujaa wa taifa

Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ndiye aliyetoa tamko hilo leo kupitia televisheni baada ya mkutano wa chama hicho na kuwa taifa hilo litaomboleza kifo hicho hadi ya mazishi.

“Chama tawala Zanu-PF kimekutana na kumtunuku heshima anayostahili Mugabe ya shujaa wa taifa,” alisema Mnangagwa akinukuliwa na AFP.

Siku tatu za maombolezi ya kitaifa zimeanza kufuatia kifo hicho. Hata hivyo, haikuelezwa mazishi hayo yatafanyika lini.

Mugabe, rais wa kwanza wa Zimbabwe aliongoza taifa hilo hadi alipopinduliwa na jeshi 2017.

BBC imeripoti kuwa licha ya kusifiwa awali kwa kupanua sekta ya afya na elimu kwa weusi walio wengi, Mugabe baadaye alitumia ghasia dhidi ya wapinzani wake na kuongoza uchumi wa taifa hilo ulioanguka vibaya.

Advertisement

Kimataifa mpiganaji huyo wa zamani alionekana kama dikteta kufuatia hatua ya jeshi kuwashambulia wapinzani wake mbali na kunyakua ardhi kutoka kwa wakulima wachache weupe ili kupiga jeki umaarufu wake miongoni mwa wapiga kura.

Uongozi wake umezua mjadala mkubwa tangu kifo chake.

Alikuwa maarufu miongoni mwa wapiga kura wengi hata katika kipindi chake cha hivi karibuni alipong'atuliwa mamlakani baada ya kumtimua kazi makamu wake Mnangagwa, ambaye baadaye alikabidhiwa madaraka na jeshi.

Mugabe alifia nchini Singapore alikokuwa anapata matibabu tangu Aprili. Mamlaka nchini humo zinashirikiana na ubalozi wa Zimbabwe kuusafirisha mwili wake kurudi nyumbani.

 

Advertisement