Zec yatangaza kuanza kuandikisha wapiga kura

Muktasari:

  • Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) imesema inatarajia kufanya kazi ya uandikishaji wapiga kura wapya hivi karibuni na kuhakikisha daftari la wapiga kura ili wasio na sifa waondolewe.

Unguja. Wakati ikiwa imebaki mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) imesema inatarajia kufanya kazi ya uandikishaji wapiga kura wapya hivi karibuni.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya sheria na uchaguzi kwa waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 17,2019 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Thabit Idarous Faina  amesema lengo la uandikishaji ni kuhakikisha kila mwenye sifa ya kupiga kura anaandikishwa.
Amesema uongozi wa Zec hivi sasa upo katika hatua za mwisho za maandalizi ya uandikishaji huo huku akiahidi wakati wowote wanaweza kutangaza tarehe ya kuanza kwa kazi hiyo.
"Niwaombe sana wale wote ambao wana haki ya kuandikishwa katika daftari la wapiga kura wajitokeze kwa wingi wakati utakapofika, hii ni haki yao kwa mujibu wa sheria za nchi," amesema .
Faina amesema mbali ya kazi ya hiyo ya uandikishaji Zec inatarajia kufanya uhakiki wa wapiga kura wote waliomo katika daftari la wapiga kura.
Amesema lengo la ni kuangalia wale ambao hawana sifa za kuwemo katika daftari hilo wanaondolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Ametaja baadhi watu ambao wanaweza kuondolewa katika daftari hilo ni waliofariki au waliokosa sifa ya kustahiki kuandikishwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za kiraia wa kuangalia chaguzi Tanzania (Tacceo), Maxin Camisana amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaweka tayari waandishi kufahamu vyema majukumu yao wakati wa uchaguzi ili kuepusha kuripoti habari za uchaguzi kinyume na sheria za tume za uchaguzi.