Ziara za Makonda Dar zazua jambo

Muktasari:

Wachambuzi wasema ni vyema viongozi kuepuka matukio yanayochochea mikusanyiko ya watu

Dar es Salaam. Ziara za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika maeneo mbalimbali zinazosababisha mikusanyiko ya watu zimeibua mjadala huku wachambuzi wakisema jambo hilo linatakiwa kuangalia kwa makini ili kuapuka maambukizi ya virusi vya corona.

Mbali na wachambuzi hao, jana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa katibu wa kanda ya Pwani, Hemed Alli kilieleza kuwa kitendo hicho kinaliingia jiji katika hatari ya kusambaa kwa virusi hivyo.

Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Dk Paul Luisulie alisema suala la kuepuka misongamano lilishatolewa ufafanuzi kwa hiyo anachofanya mkuu wa mkoa na viongozi wengine kinaweza kutafsiriwa kisiasa.

Alisema tahadhari moja ya kuepuka ugonjwa wa Covid-19 ni kukaa mbali na mosongamano lakini inapotokea kiongozi mwenyewe anasababisha mikusanyiko inaleta picha kwamba bado watu hawajali.

“Ushauri wangu, ni vizuri viongozi wakaepuka matukio yanayochochea mikusanyiko inayosababisha misongamano itakayochangia maambukizi ya gonjwa hili hatari duniani,”alisema.

Mhadhiri wa UDOM, Frank Tilly alisema kitendo cha kiongozi huyu kuhamasisha mikusanyiko ni kama kwenda kinyume na kanuni za kuzuia corona.

Alisema zuio la misongamano isiyo ya lazima lilishatolewa na Serikali ili kupunguza uwezekano wa corona kuenea kwa kasi.

“Ugonjwa huu umeshatangazwa kuwa upo katika Jiji la Dar es Salaam, kama unawakusanya watu ambao hujui labda walikutana na waathirika kwa namna moja ama nyingine kama kiongozi unakuwa ndiyo chanzo cha kuenea na siyo uzuia,”alisema.

Alipoulizwa kuhusu utaratibu huo, katibu mkuu Wizara ya Afya Zainab Chaura alisema kila mtu ana maeneo yake ya kufanya kazi.

Hata hivyo, hakutaka kulizungumzia zaidi suala hilo na badala yake alisistiza wananchi kuchukua tahadhari ikiwamo kunawa mikono kwa maji na sabuni pamoja na kuepuka misongamano.

Hivi karibuni wakati Makonda akizungumza na wananchi katika kituo cha daladala cha Makumbusho aliwataka kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwamo kukaa nyumbani kama hakuna ulazima wa kutoka.