Zitto amjibu Ndugai mkopo wa Benki ya Dunia

Muktasari:

Mbunge Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) nchini Tanzania, Zitto Kabwe amepinga kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyehoji sababu za yeye kuiandikia barua Benki ya Dunia (WB) akitaka Tanzania inyimwe mkopo wa elimu.

Dar es Salaam. Mbunge Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) nchini Tanzania, Zitto Kabwe amepinga kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyehoji sababu za yeye kuiandikia barua Benki ya Dunia (WB) akitaka Tanzania inyimwe mkopo wa elimu.

Zitto amesema hakuna tofauti ya kisera katika suala la watoto wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 31, 2020 bungeni mjini Dodoma baada ya maelezo ya naibu waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara aliyekuwa akijibu swali la Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul aliyetaka Serikali iingize suala la ujenzi wa nyumba za walimu katika bajeti.

Akizungumza baada ya majibu ya Waziri Waitara, Ndugai amesema Zitto kuandika barua hiyo ni tofauti za za kisera, lakini kuzuia fedha za Benki ya Dunia ni kwenda mbali zaidi.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Zitto ambaye yupo nchini Uingereza amesema, “hakuna tofauti ya kisera katika suala la watoto wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo. Ilani ya CCM iliahidi hilo, wananchi mwaka 2015, vyama vya Upinzani viliahidi hilo na wananchi 2/3 wanaunga mkono hilo.”

Zitto ambaye pia ni kiongozi wa ACT Wazalendo, amesema hata ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 inataka watoto wa kike waliopata ujauzito warudi shuleni.

“Asilimia 71 ya wananchi wanaunga mkono watoto wa kike waliopata ujauzito kuendelea na masomo. Ilani ya CCM pia inataka warudi shule,” amesema.