Zitto asema atampigia kura Lissu

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe

Muktasari:

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe leo Ijumaa Oktoba 16, 2020  amesema atampigia kura mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu katika uchaguzi mkuu wa  Oktoba 28, 2020.

Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe leo Ijumaa Oktoba 16, 2020  amesema atampigia kura mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu katika uchaguzi mkuu wa  Oktoba 28, 2020.

Septemba 8, Lissu alifanya kampeni Zanzibar kueleza jinsi mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad alivyo na ushawishi na wezo wa kushinda na alipokuwa mjini Kigoma Septemba 19, 2020 alitangaza chama hicho kumuunga mkono Zitto katika ubunge wa jimbo hilo.  

Akizungumza leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Bangwe Kigoma mjini, Zitto anayegombea ubunge Kigoma mjini amesema  licha ya chama chake kuweka wagombea katika ngazi zote kuanzia urais hadi udiwani, uongozi wa chama hicho uliona umuhimu wa kushirikiana na vyama vingine.

“Kamati ya uongozi ya chama chetu imeshauriana na kuona kuwa huu ni mwaka wa kihistoria kwa Watanzania, mwaka wa kuamua hatma ya maisha yao.”

“Ni mwaka wa Watanzania kuchagua kiongozi atakayerejesha furaha katika maisha yao, atakayeheshimu katiba ya nchi yao, atakayejali maendeleo ya watu badala ya vitu, atakayeheshimu wanawake wa Tanzania na atakayerejesha uhuru wa watu,” amesema.

Ameongeza, “sisi ACT Wazalendo hatupo tayari kuwa kizuizi cha safari hii ya mabadiliko, nami kama kiongozi wa chama ninao wajibu wa kulieleza hilo kwa uwazi kwa niaba ya viongozi wenzangu wa kamati ya uongozi.”

Zitto aliyekuwa amesitisha kampeni zake baada ya kupata ajali ya gari huko Kalya, jimbo la Kigoma Kusini  Oktoba 6, 2020 amewataka wafuasi wa chama hicho kuwapigia kura wagombea wa ACT Wazalendo katika majimbo mbalimbali na kama hakuna wagombea wa chama hicho wawapigie wagombea wa vyama vya upinzani.

“Kama kuna wagombea wengine wa vyama vya upinzani, ACT Wazalendo tunawaomba mpigie kura mgombea wa chama cha upinzani mwenye nguvu zaidi ili kutokutawanya kura,” amesema Zitto.

Kuhusu urais amesema, “kwa nafasi ya Rais mimi Zitto Zuberi Ruyagwa Kabwe nitapiga kura yangu kwa Tundu Antipas Mughwai Lissu. Huyu ndiye mgombea wa upinzani ambaye ana nguvu ya kumshinda mgombea wa chama tawala.”

“Amefanya kampeni nchi nzima, mwitikio wa wananchi kwake ni mkubwa sana, ameeleza kwa ufasaha dhamira yake ya kuleta mabadiliko na sina mashaka na dhamira hiyo, pamoja na anayotaka kuyafanya kama Rais, ni mambo hayo ndiyo yaliyonipa msukumo wa kumpigia kura Lissu.”