Zitto ataja sababu kusoma vitabu vichache mwaka 2019

Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe

Muktasari:

Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe amesema mwaka 2019 amesoma vitabu vichache tofauti na miaka iliyopita kutokana na muda mwingi kuutumia mahakamani kusikiliza kesi zinazomkabili.

Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe amesema mwaka 2019 amesoma vitabu vichache tofauti na miaka iliyopita kutokana na muda mwingi kuutumia mahakamani kusikiliza kesi zinazomkabili.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini amesema mwaka 2019 amesoma vitabu 34, “mwaka 2018 nilisoma vitabu 49 na mwaka 2017 vitabu 39.”

Zitto ameeleza hayo leo Ijumaa Desemba 20, 2019 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari. Kiongozi huyo wa ACT- Wazalendo amekuwa akitoa orodha ya vitabu alivyosoma kila mwaka na mara kadhaa amenukuliwa akisema anafanya hivyo kuwajengea watu wengine utamaduni wa kusoma vitabu kuongeza ujuzi na maarifa.

Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu katika kesi ya uchochezi anayodaiwa kuyatenda Oktoba 28, 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Kijitonyama, Dar es Salaam. Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi.

 

Maelezo ya Zitto kuhusu vitabu alivyosoma

Mwaka 2019 nimejaaliwa kusoma vitabu 34 (2018:49 na 2017:36+3). Ni sahihi kuwa idadi imepungua sana, hii ni kwa sababu shughuli nazo zimekuwa nyingi, haswa masuala ya ujenzi wa chama na kuhami demokrasia. Mwaka 2019 ndio mwaka nimekanyaga mahakamani mara nyingi zaidi kuliko wakati wowote wa maisha yangu. Majukumu yanapozidi, muda wa kujisomea unapungua. Hata hivyo nashukuru sana nimejikongoja mpaka kufikia vitabu 34.

Ingizo jipya ni riwaya za mwandishi wa Kituruki Orhan Pamuk ambaye nimesoma vitabu vyake 4 mwaka huu. Amenifanya kupenda kusoma kazi za waandishi wengine kutoka Uturuki kutokana na riwaya zake zenye mchanyato wa masuala ya Siasa za Uturuki, utamaduni, mapenzi na maisha ya watu kiujumla. A Strangeness in Mind ndio ilinivutia kuliko zote katika Riwaya za Pamuk nilizoorodhesha hapa. Hii ni riwaya inayoeleza maisha ya kijana Mevlut aliyetoka shamba na kuhamia mjini na namna maisha yalivyobadilika kwa kasi. Ni hadithi inayoonyesha tamaduni za kituruki kuhusu ndoa na mahusiano ya ndugu na familia. Kitabu hiki kitakufanya uione Uturuki na mapinduzi ya kijeshi yalivyoigubika mwaka hadi mwaka, pamoja na mtanziko wa Siasa zenye kuheshimu misingi ya Dini au kufuata umagharibi. Riwaya za Pamuk nilizosoma ni pamoja na;

 

1.    Orhan Pamuk - Snow

 

2.    Orhan Pamuk - Silent House

 

3.    Orhan Pamuk - A Strangeness in Mind

 

4.    Orhan Pamuk - Instanbull

 

Nilisoma pia Riwaya nyengine kadhaa zikiwemo kazi za watunzi mliozoea kuwaona kama Jefrey Archer na John Grisham katika orodha zangu za miaka ya hivi karibuni. Pia nilimsoma Mzee Makaidi, kazi yake aliyoandika mingi nyuma. Mwaka huu nimevutiwa sana na kazi za mtunzi wa kitanzania anayechipukia Bwana Lello Mmasy. Riwaya na Mimi na Rais ilinikosesha usingizi kwani sikutamani kuacha kuisoma. Ni Riwaya iliyosadifiwa vizuri na kwa ubunifu mkubwa huku ikichora picha halisi yenye kuvutia msomaji.

Riwaya hii naifananisha na ile ya A Man of The People ya Chinua Achebe (kwa ubunifu na labda utabiri). Nchi ya Stanza na Rais wake Bwana Costa aliyekuwa anaharibu Uchumi wa Taifa lake, katika riwaya hii,  inaweza kuwa ni nchi yeyote ya Afrika katika hali ya sasa.

Nilifurahi pia kusoma kazi ya Mama Fatma Jinja iitwayo The Shirazi Enigma kwani ni hadithi yenye historia kubwa ya Zanzibar. Ukitaka kujua usasa na uchangamano wa watu wa mataifa mengi Zanzibar soma hadithi ya Salwa katika Riwaya hii. Bwana Abdulrazak Gurnah pia anasimulia hadithi katika historia ya Zanzibar pia. Kazi yake niliyoorodhesha hapa ni historia ya Siasa na familia za Zanzibar katika miaka ya Sabini na Themanini. Mtunzi wa Riwaya Helmut Zell kutoka Ujerumani pia alinivutia kazi yake ya Black Money in Dar. Ukisoma Riwaya hiyo unakumbuka mtifuano wa sakata la Escrow mwaka 2014. Kama kwa Mmasy, nilijisoma pia kwa Zell. Riwaya nilizosoma ni pamoja na;

 

5.    Jeffrey Archer - Nothing Ventured

 

6.    Abdulrazak Gurnah - Gravel Heart

 

7.    Fatma Jinja - The Shirazi Enigma

 

8.    E J E Makaidi - The Serpent: Hearted Politician

 

9.    Helmut Zell - Black Money in Dar es Salaam

 

10. Lello Mmassy - Mimi na Rais

 

11. Jeniffer M Makumbi - Kintu

 

12. John Grisham - The Guardians

 

Kama kawaida, napenda historia. Hivyo mwaka huu nilisoma vitabu vya historia kadhaa ili kupata maarifa ya tulipotoka ili niweze kutafakari huko tunakokwenda. Vitabu vya historia nilivyosoma ni pamoja na;

 

13. W H Ingrams - Zanzibar: Its History and Its People

 

14. Judith Listowel - The Making of Tanganyika

 

15. Linda Pappas Funsch - Oman Reborn: Balancing Tradition and Modernisation

 

16. A Monument to China - Africa Friendship: Firsthand Account of the Building of The TAZARA

 

17. Amilcar Cabral - Unity and Struggle

 

18. Paul Kenyon - Dictatorland

 

19. Yuval Noah Harari - Sapiens: A Brief History of Humankind

 

Mwaka huu tumebahatika kupata vitabu vya baadhi ya Viongozi wetu nchini. Rais wa Awamu ya Tatu Mzee Benjamin Mkapa ameandika Wasifu wake. Amesimulia maisha yake. Kabla ya hapo Mzee Njelu Kasaka, aliyekuwa Mbunge na Katibu wa Kundi la G55 lililotaka Serikali ya Tanganyika alitoa kitabu chake pia. Vitabu muhimu sana katika kuifahamu Tanzania ilipotoka na ilipo kupitia maisha ya wanasiasa hawa. Nimefurahi sana kusoma vitabu vyao. Pamoja nao pia nilisoma vitabu vya watu wengine kama vile Hashil Seif ambaye alishiriki mapinduzi ya Zanzibar.

Kitabu cha Balozi Wilibrod Slaa kinaeleza maisha yake na pia nini kilitokea katika chama cha CHADEMA mwaka 2015. Sio kitabu cha kupuuza kwani kina mafunzo mengi kwa wanasiasa. Nasikitika kuwa Balozi Slaa alichagua ya kutoandika kwani labda kupitia kwake ningeweza kujua haswa ushiriki wake katika kufukuzwa kwangu kwenye chama ambacho yeye alikuwa Katibu Mkuu. Nilikinunua ili nisome suala hilo, bahati mbaya hakusimulia mkasa ule wa Zitto na Kitila.

A Son of Two Countries cha Casmir Rubagumya ni wasifu wa Mtanzania mwenye asili ya Rwanda ambaye aliishi maisha ya ukimbizi na wazazi wake, kusoma mpaka kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu na hatimaye kustaafu. Alipata uraia wa kuandikisha na kuitumikia Tanzania kwa weledi wake wote. Licha ya kubembelezwa kurudi Rwanda baada ya mauaji ya kimbari, aligoma na kuendelea kuwa Mtanzania tofauti na wenzake wengi wa aina yake ambao waliamua kurudi Rwanda. Ni simulizi ya maisha yenye kusisimua na mafunzo. Ni Kitabu kimojawapo ambacho nilipokishika sikukiacha mpaka namaliza. Wasifu na Tawasifu nilizosoma ni pamoja na;

 

20. Benjamin W Mkapa - My Life, My Purpose

 

21. Njelu Kasaka - Maisha, Siasa and Hoja ya Tanganyika: G55

 

22. Hashil Seif Hashil - Mimi, Umma Party na Mapinduzi ya Zanzibar

 

23. Willibrod P Slaa - Nyuma ya Pazia: CHADEMA ilivyosalitiwa 2015

 

24. Casmir M Rubagumya - A Son of Two Countries

 

25. Sergey Plekhanov - Sultan Qaboos Bin Said A Said: A Reformer on the Throne

 

26. Ken Saro-Wiwa - A Month and a Day: A Detention Diary

 

Mchanganyiko wa vitabu mbalimbali kama kawaida. Ni katika kuongeza maarifa au kurutubisha itikadi ya Ujamaa. Pia katika kujifunza makosa ya wengine ili kutorudia makossa hayo. Vitabu mchanganyiko mwaka huu ni pamoja na;

 

27. James Brent Styan - The Bosasa Billions

 

28. Christine Berry + Joe Guinan - People Get Ready: Preparing for a Corbyn Government

 

29. P. Anyang’ Nyong’o - Presidential or Parliamentary Democracy in Kenya?

 

30. Greg Mills et al - Democracy works

 

31. Nick Robinson et al - The Power of Journalists

32. Douglas Rogers - Two Weeks in November: The Astonishing Inside Story of the Operation that Toppled Mugabe

 

33. Nanjala Nyabola - Digital Democracy, Analogue Politics

Zawadi kubwa niliyopata mwaka huu ni kitabu kinachoeleza Aya za Qur’an Tukufu na muktadha wa kila Aya katika kushuka kwake. Ni kitabu kinachokaa pembeni ya Kitanda changu kwa ajili ya marejeo ya mara kwa mara. Wanazuoni wa mirengo yote ya Dini ya Kiislam wameshiriki katika kuandika ‘comentaries’ za kitabu hiki.

 

34. Sayyed Hossein Nasir - The Study Quran

Mwaka huu ninatangaza kitabu changu cha Mwaka, yaani Kitabu kilichonivutia zaidi kuliko vyote nilivyosoma mwaka huu. Kitabu changu cha Mwaka 2019 ni Two Weeks in November cha Bwana Douglas Rogers. Kitabu hiki kinaeleza namna Watu mbalimbali waliokuwa maadui na marafiki, waliokuwa wakiviziana kuuana na wapinzani wakubwa, walivyoshirikiana kumwondoa madarakani Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe mwezi Novemba mwaka 2017.

Ni kitabu cha matukio ya kweli ambayo huwezi dhania ni kweli, unaweza kudhani ni hadithi tu. Licha ya kwamba kuondolewa kwa Mugabe madarakani hakujaleta ahueni kwa wananchi wa Zimbabwe, mbinu, mikakati na mafunzo ndani ya Kitabu hiki ni somo tosha kwa wapigania demokrasia kote Afrika. Hiki ni kitabu ambacho utakirudia hata mara 10 bila kuchoka.

Kila Rais wa Afrika, kila Mkuu wa Majeshi, kila Kiongozi wa Upinzani na kila mwanasiasa mwenye kujitambua asome kitabu hiki. Akifanye rejea yake ya mara kwa mara. Wiki 2 za Novemba 2017 zaweza kutokea katika nchi yeyote ambayo Viongozi wake hawazingatii demokrasia, utawala wa sheria, Utu na mshikamano katika kuendesha Taifa. Tafuta nakala yako.

Nawatakia kheri katika kumaliza mwaka 2019 na kila la kheri katika mwaka 2020. Nawashawishi kupata muda wa kujisomea japo kitabu kimoja kila mwezi. Kusoma ni kurutubisha ubongo.