Watano wafa ajalini wilayani Rufiji lori likiteketea kwa moto

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Onesmo Lyanga

Muktasari:

Watu watano wamekufa na mmoja akijeruhiwa baada ya magari mawili kugongana na kupinduka Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani.

Dar es Salaam. Watu watano wamekufa na mmoja akijeruhiwa baada ya magari mawili kugongana na kupinduka Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani.

Akizungumza leo Jumamosi Agosti 31, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Onesmo Lyanga amesema ajali hiyo imehusisha lori la kampuni ya Dangote lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mtwara likiwa limepakia malighafi ya kutengeneza saruji.

Lori hilo liligongana na gari dogo aina ya Toyota Premio lililokuwa likitoka kwenye nyumba za walimu wa Shule ya Sekondari ya Kibiti eneo la Kinyanya.

Amesema gari hilo liliingia barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda Mtwara bila kuzingatia sheria na kugongana na lori hilo.

Kamanda Lyanga amesema  baada ya magari hayo kugongana gari la Dangote lilipoteza mwelekeo na kugonga nguzo ya umeme na nyaya kuanguka iliyosababisha moto ulioshika katika lori hilo na kusababisha vifo vya watu wanne.

Amesema mmoja kati ya watu wawili waliokuwa katika gari hilo dogo alifariki  wakati akipatiwa matibabu wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Kamanda Lyanga amesema kuwa miili imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Mkuranga.

Amesema lori hilo lilikuwa na watu wanne akiwemo dereva na wote waliteketea kwa moto, kwamba hadi leo saa 6 mchana miili yao ilikuwa haijatambuliwa.

Amesema abiria aliyekuwa katika gari dogo alikatika vidole vya mguu na damu ikawa inavuja nyingi, alifariki dunia baada ya kufikishwa katika Hospitali ya misheni ya Chubwi, “dereva wa gari hilo anapatiwa matibabu katika hospitali hiyo.”