Upungufu wataalam dawa za usingizi watajwa kuathiri upasuaji salama Tanzania

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa  Muhimbili (MNH),  Profesa Lawrence Mseru

Muktasari:

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa  Muhimbili (MNH),  Profesa Lawrence Mseru amesema upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi nchini Tanzania unaweza kuathiri upasuaji salama.

Dar es salaam. Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa  Muhimbili (MNH),  Profesa Lawrence Mseru amesema upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi nchini Tanzania unaweza kuathiri upasuaji salama.

Profesa Mseru amesema hayo leo Alhamisi Februari 20, 2020  katika  ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya madaktari ambayo Rais John Magufuli ndio mgeni rasmi.

Amesema kuna changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa katika fani zote, ni muhimu kwa Taifa kuwekeza kwenye elimu na ujuzi ili kukabiliana na tatizo hilo.

“Upungufu huu sio wa fani ya madaktari peke hata katika fani nyingine za wauguzi na wafamasia. Pia wataalamu wa kutoa dawa za usingizi upungufu ni mkubwa sana jambo linaloweza kuathiri utoaji huduma wa upasuaji salama,” amesema.

Ameishukuru  ameishukuru Serikali kutoa fedha maalumu Sh5 bilioni kwa ajili ya kuwasomesha madaktari bingwa 600 katika kipindi cha miaka sita ili kukabiliana na tatizo hilo.

Amesema Serikali imewekeza kwenye raslimali watu wakiwamo madaktari bingwa na madaktari bingwa wabobezi ili kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi.

Profesa Mseru ambaye ni mlezi wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) amesema hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeanzisha huduma ambazo awali zilikuwa zinafanyika nje ya nchi na kuokoa Sh34 bilioni.

“Huduma hizi ni pamoja na upandikizaji wa figo, vifaa vya usikivu kwa watoto wadogo. Mtoto mdogo aliyezaliwa kiziwi akipewa huduma anaweza kuepuka changamoto ya uziwi kwenye maisha yake,” amesema.

Amesema huduma hizo zinatolewa pia kwenye hospitali nyingine ikiwamo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Bugando na nyingine.

Ameishukuru Serikali kuwekeza katika kuwasomesha madaktari ili kukabiliana na changamoto.

Maadhimisho hayo yanafanyika wakati MAT ikitimiza miaka 55 tangu kilipoanzishwa.