Aliyekuwa na kesi ya uhujumu uchumi ahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya Sh 270 milioni.

Muktasari:

Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, imemhukumu, Waziri Mizogi, kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya zaidi ya Sh 270milioni, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin na Cocaine.

Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, imemhukumu, Waziri Mizogi, kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya zaidi ya Sh 270milioni, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin na Cocaine.

Pia mahakama hiyo, imeamuru dawa hizo za kulevya ziteketezwe katika kiwanda cha Saruji cha Jijini Mbeya.

Mizogi alikuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 66/2015, kwa kukutwa na  kusafirisha dawa za kulevya, kinyume cha sheria.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Dk Adam Mambi, baada ya mshtakiwa huyo kutiwa hatiani, katika makosa mawali  ya kusafirisha dawa za kulevya.

Jaji Dk Mambi amesema mshtakiwa huyo, ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mambi alisema katika shtaka la kwanza, ambalo ni kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 1645.89, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya Sh 73,873,350.

 

Jaji Mambi alisema katika shtaka pili, ambalo ni kukutwa na kusafirisha dawa za kulevya aina Cocaine zenye uzito wa gramu 547.21, mshtakiwa atalipa faini ya Sh 197,082,450.

Dk Mambi alisema adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo hicho na kulipa faini zote.

Alisema kama mshtakiwa hajaridhika na adhabu hiyo anaweza kukata rufaa.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Achiles  Mulisa aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya Mizogi.

Katika ya kesi ya msingi, Mizogi  anadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 4, 2012 katika nyumba ya kulala wageni ya Nice Shirez, iliyopo eneo la Tunduma wilaya ya Momba, mkoani Songwe.

Mshtakiwa siku ya tukio, saa 5 asubuhi,  alikutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin gramu 1645.89 na Cocaine gramu 547.21 chumbani kwake, kinyume cha sheria.