Sakata la mameya wa Chadema kuondolewa madarakani latinga bungeni

Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa akichangia Mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Rais Tawala na Serikali za Mitaa ya Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Iringa Mjini(Chadema) nchini Tanzania, Peter Msigwa amelalamikia bungeni utaratibu uliotumika kuwaondoa katika nafasi zao mameya wawili wa Iringa Mjini na jiji la Dar es Salaam.

Dodoma. Sakata la kuondolewa kwa mameya wawili wa halmashauri zilizokuwa zikiongozwa na Chadema limetinga bungeni ambapo Mbunge wa Iringa Mjini, (Chadema), Peter Msigwa amesema hata barua ya kukata rufaa iliyoandikwa kwa Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo haijajibiwa.


Msigwa aliwataja walioondolewa kuwa Meya wa Iringa Mjini, Alex Kimbe na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita ambaye ameandika barua ya rufaa mwezi mmoja uliopita.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2020/2021, leo Alhamisi Aprili 9, 2020 Msigwa amesema Manispaa ya Iringa ni miongoni mwa manispaa bora na nzuri nchini.


Amesema katika kipindi cha miaka mitano akiwa mbunge wamekuwa na hati safi, wamekusanya mapato, wamepatiwa zawadi ya usafi na madiwani wengine kufika kujifunza chini ya uongozi wa meya huyo.


Amesema Serikali imekuwa ikijinasibu kukataa wizi lakini wamekuwa na meya huyo ameweza kusimamia jambo hilo katika kipindi chake cha uongozi.
“Kanuni zinasema ukitaka kumuondoa meya lazima umuondoe kwa theluthi mbili lakini uongozi wa mkoa wamefanya fitina tena kwa fujo wamemuondoa meya katika uongozi mtu ambaye anafanya kazi,”amesema.


Amesema meya huyo ambaye amekuwa mfano nchini ameondolewa kwa tuhuma za uongo.
Amesema waliomtoa ni madiwani 14 kati ya 26 na kuhoji waliipataje theluthi mbili ya kura ili kumuondoa kikanuni.


Msigwa amesema waliomshtaki meya huyo hawaonekani na hakupewa muda wa kujitetea kwa mujibu wa kanuni.
 “Tunajaribu kudai hao waliomshtaki ni wakinani fujo zinafanyika. Tunawasiliana na vyombo vinavyohusika hakuna msaada. Hawa watu hawakujichagua wenyewe. Tunaendeshaje hii nchi, hii nchi inakuaje kwa uonezi wa namna hii.


Eti fisadi ana ka-spacio ambacho alikuwa nacho hata kabla hajawa diwani. Najua unaweza ukaja hapa ukasema taratibu zinasema akate rufaa lakini Meya wa Dar es Salaam ameandika barua zaidi ya mwezi hujamjibu,”amesema.


Amesema Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi ameshindwa kufanya kazi na hivyo anatafuta sababu na hazipo na kumuomba Jafo kulitafutia ufumbuzi.