CCM kuwawekea pingamizi wagombea wa upinzani uchaguzi Serikali za mitaa

Thursday November 7 2019

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Hamphrey

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,Hamphrey Polepole akizungumza na wanahabari kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama hicho  kitawawekea  pingamizi wagombea wa vyama vya upinzani kwa madai kuwa wengi hawana sifa.

Polepole ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 7, 2019 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya CCM katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Katika mchakato wa uchaguzi huo vyama vya upinzani vimelalamika kufanyiwa hujuma na ukiukwaji wa kanuni hali iliyosababisha wagombea wake kuenguliwa.

Polepole amesema wagombea wa upinzani waliopitishwa hawajui kusoma, wengine wamepitishwa katika maeneo ambayo hawaishi.

 “Wale waliobaki (wapinzani) wamewekewa mapingamizi ya kufa mtu, hawana sifa. Wengi wao hawaishi kwenye mitaa ambayo wanagombea, hawajui kusoma, wengine hawana kazi,” amesema Polepole.

Mwanasiasa huyo amebainisha kwamba wanachama wa CCM milioni 15 wamejiandikisha kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo wana uhakika wa kupata ushindi kwa kutegemea kura za wanachama wake.

Advertisement

Amesema katika maeneo ambayo wagombea wa vyama vya upinzani wameenguliwa, maana yake ni kwamba CCM imepita bila kupingwa.

Amesema si mara ya kwanza CCM kupita bila kupingwa kwa sababu chama hicho kimepita bila kupingwa mwaka 2014 katika wilaya za Monduli, Korogwe, Bagamoyo, Lushoto, Handeni na Kongwa.

 “Ni kweli mwaka huu tutashinda sana kwa sababu serikali ya awamu ya tano inafanya kazi kubwa, hospitali kila wilaya zimejengwa, elimu sasa ni bure, umeme unapatikana mpaka vijijini. Kwanini tukose ushindi, hakuna sababu,” amesema Polepole.

 

 

Advertisement