Sunday October 16 2016

By Julieth Ngarabali, Mwananchi [email protected]

Chalinze. Zahanati ya Vigwaza iliyopo wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani ambayo ilifunguliwa miaka mitatu iliyopita, haijawahi kupata mgawo wa dawa kutoka kwa mamlaka husika. 

Kutokana na hali hiyo, Diwani wa Vigwaza wilayani humo, Mohsin Bharwani ameamua kutoa msaada wa vifaatiba na dawa mbalimbali muhimu zenye thamani ya zaidi ya Sh4.5 milioni kwa ajili ya zahanati hiyo na nyingine ya Ruvu Darajani.

Akikabidhi dawa hizo kwa waganga wa zahanati hizo, Bharwani alisema ameguswa kutoa msaada huo ili kupunguza malalamiko ya wananchi wanaodai Serikali imeshindwa kuwapelekea dawa.

Ofisa Tabibu wa Zahanati ya Vigwaza, Alexander Ngalawa alisema mahitaji ya dawa ni makubwa kutokana na wingi wa wagonjwa wanaowahudumia kutoka vijiji  vya Buyuni, Vigwaza, Kwazoka na Mnindi.

 

Advertisement