NYANZA: Ajipiga risasi, aacha ujumbe kwa baba mkwe

Monday August 10 2015

By Jovither Kaijage, Mwananchi

Ukerewe. Mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya Jitegemee ya Mwanza, Stephano Imbuhu (39), amejiua kwa kujipiga risasi kutokana na kile kinachodaiwa mgogoro katika ndoa.

Habari zilizopatikana kutoka kituo chake cha kazi, Kisiwani Kweru Mto, Ukerewe zinadai kuwa marehemu alijiua juzi saa tisa alasiri baada ya mkewe, Edita Makalanga  akiwa na watoto wao wawili  kuondoka nyumbani na kwenda kusikojulikana.

Inadaiwa kuwa, Edita aliondoka nyumbani bila kumtaarifu mume wake na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi haikupatikana.

Majirani walidai kuwa uamuzi wa mke kuondoka bila kutoa taarifa, ulimchukiza marehemu na kuamua kujipiga risasi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo  alithibitisha kutokea tukio hilo.

Alisema marehemu alijiua kwa kutumia bunduki aina ya Rifle yenye namba 70526 mali ya kampuni aliyokuwa akifanya kazi.

Advertisement

Kamanda Mkumbo alisema marehemu alijipiga risasi kifuani akiwa chumbani.
“Kabla ya kujiua, aliandika ujumbe kupitia simu yake ya mkononi akieleza kuwa ameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na mgogoro wa ndoa na mke wake,” alisema Kamanda Mkumbo.

Alisema ujumbe wa kuamua kujiua aliutuma kwa baba mkwe wake, baadhi ya ndugu zake na rafiki yake.

Kamanda Mkumbo alisema ujumbe huo ulikutwa kwenye simu yake ya mkononi.

Ujumbe huo uliandikwa hivi: “Baba mkwe wangu, sistahili kuishi  duniani kwa sababu ya mwanao  kanifanya mimi kama mwanamke na yeye kuwa mwanaume. Naomba uhudhurie mazishi yangu na usiwaache wanangu, Gadina na  Majid. Asante.”

Mlinzi huyo alikuwa akilinda mali za mfanyabishara mmoja kutoka Kisiwa cha Kweru Mto, aliyetajwa kwa jina la Osward Mwandumisya.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ukerewe, Ally Mkalipa alisema amesikitishwa na tukio hilo na kuwataka wananchi kuomba msaada wa ushauri wanapokumbana na matatizo ya kifamilia.

“Kwenye maisha kuna matatizo mengi tunakumbana nayo, mengine yako nje ya uwezo, lakini hata hivyo hakuna sababu ya kujiua. Nawaomba wananchi kutafuta ushauri wanapokabiliwa na matatizo mbalimbali,” alisema Kamanda Mkalipa.

Advertisement