Mwigulu awapa raha wafanyabiashara Tanga

Monday January 19 2015

By Burhani Yakub, Mwananchi

Tanga. Ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba imewafurahisha wafanyabiashara katika gulio la Tangamano baada ya kutangaziwa rasmi kwamba hawatahamishwa katika eneo hilo.

Wafanyabiashara hao ambao hufanya biashara zao Tangamano siku za Jumanne, Alhamisi na Jumamosi, walitakiwa kuondolewa mapema mwezi huu na Halmashauri ya Jiji la Tanga na kupelekwa Mwahako nje kidogo ya mji.

Tangazo hilo liliwasilishwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi waliokaa jukwaani na Mwigulu aliyewasili uwanjani hapo kwa helikopta kuzungumza na wananchi.

Magalula alipewa nafasi hiyo na Mwigulu aliyepenyezewa kikaratasi na wafanyabiashara wa gulio hilo wakimlalamikia kwamba wamepewa amri na Halmashauri ya Jiji kuhamia Mwahako sehemu waliyodai ni nje ya mji na itakuwa vigumu kwa wanunuzi kufika.

Mara baada ya kuhutubia Mwigulu ambaye aliambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma alilazimika kurejea katika kipaza sauti na kumtaka Magalula ajibu malalamiko yaliyoandikwa ndani ya karatasi iliyomfikia jukwaani hapo.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM pia aliwahimiza wakazi wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kwenye uboreshaji wa daftari la wapigakura ili waweze kutumia haki yao kikatiba ya kupata sifa ya kupigia kura maoni Katiba inayopendekezwa pamoja na uchaguzi mkuu ujao.

Advertisement