Johari: Bila milioni tano sitoki kwenye matembezi
Muktasari:
- Johari mbaye amekuwa akijijengea taswira ya kujiamini na kujithamini, amesisitiza kwa sasa hawezi kufanya jambo lolote bila kuweka mbele thamani yake, akiamini kila anachofanya kina uzito unaostahili kuheshimiwa.
MSANII wa Bongo Movie, Johari ameonyesha thamani yake hata katika mambo yanayoonekana kuwa ya kawaida ikiwamo akiwa matembezi.
Johari mbaye amekuwa akijijengea taswira ya kujiamini na kujithamini, amesisitiza kwa sasa hawezi kufanya jambo lolote bila kuweka mbele thamani yake, akiamini kila anachofanya kina uzito unaostahili kuheshimiwa.
Akifunguka kwa msisitizo, alisema, “Watu wanachukulia poa sana mambo, lakini ukweli ni hata muda wangu una thamani kubwa, mimi siwezi kutoka tu kwenda matembezini bila sababu ya msingi au bila kuona thamani yangu, bila milioni tano, sitoki hata kwenye matembezi, watu waelewe kila kitu ninachofanya sasa kina hadhi yake.”
Kauli hiyo ya Johari inagusa hata maisha ya kawaida nje ya kazi kuhusu mipaka kati ya maisha binafsi na thamani ya msanii.
Katika ufafanuzi wake, Johari alieleza hatua hiyo ni sehemu ya kujilinda na kuhakikisha hatumiki vibaya au kupoteza muda kwenye mambo yasiyokuwa na faida kwake.
“Nilipitia mengi hadi kufika hapa nilipo. Sasa hivi najua thamani ya muda wangu, nguvu zangu na jina langu. Siwezi kurudi nyuma kwa kufanya vitu bila mpangilio au bila kuona faida yake kwa maisha yangu.”
Hata hivyo, ameonekana kuwa thabiti kwenye msimamo wake, akihitimisha kwa kusema, “Sio kila mtu ataelewa, lakini wale wanaojua thamani yao watanielewa vizuri sana.”
Johari mbali na kuigiza pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Empire Lokoma na mtayarishaji wa tamthilia.