Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huwa tunamtafuta MVP au mchezaji bora wa msimu?

ZENGWE Pict


NI nadra sana kwa mashabiki na hata waandishi wa habari kukubaliana na ushindi wa mchezaji katika tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu, tuzo ambayo huchanganywa na ile ya Mchezaji Mwenye Thamani Kuliko Wote (MVP).


Pengine ni kwa kutumia majina yote mawili kwa fikra ni dhana moja ndiyo sababu ya wengi kutokubaliana na mshindi wa tuzo hiyo na pengine ni kutojua na pengine ya mwisho ni ile ya ushabiki wa Simba na Yanga.


Mchezaji Bora wa Msimu huangalia zaidi mchezaji anayefanya vizuri au aliye kwenye ubora, wakati MVP huangalia zaidi ni kwa jinsi gani mafanikio ya timu yanamtegemea mchezaji anayeshindania tuzo hiyo.

Hata hivyo, tafsiri, vigezo vya kupiga kura na utamaduni wa tuzo hutofautiana kwa kila mchezo kwa kuwa michezo mingine kama mpira wa kikapu na kriketi inategemea zaidi takwimu.

ZENG 05

Mchezaji Bora wa Msimu huangalia zaidi kiwango cha mchezaji msimu mzima bila ya kujali kama timu yake ilitwaa ubingwa ama kulikuwa na msaada kutoka nguvu za nje.

Dhana hii hutumika zaidi katika soka kama England, ambako msimu huu Declan Rice wa Arsenal ametwaa tuzo hiyo ingawa si kwa kuiongoza Arsenal kutwaa ubingwa wake wa kwanza katika miaka 22.

Mara nyingi wapigakura huangalia jinsi mchezaji alivyozungumziwa msimu mzima, mchango wake kwa jumla katika mabao ambayo timu yake ilifunga na ustadi wake aliouonyesha msimu mzima.

ZENG 04

MVP ni dhana inayotumika kuangalia umuhimu wa mchezaji katika mafanikio ya timu, kiasi kwamba asipokuwepo kiwango cha timu hushuka kwa kiasi kikubwa. Hii ni dhana inayotumika zaidi katika michezo kama mpira wa kikapu kama Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA) au Ligi Ya Mpira wa Miguu Aina ya Kimarekani (NFL).

Dhana hii huangalia zaidi uwezo wa mchezaji kuwabeba wachezaji wenzake na kuiwezesha timu kushinda. Wachezaji ambao wako kwenye timu inayoshindwa hukosa sifa ya kuingia kwenye ushindani wa tuzo hii hata kama takwimu binafsi ni nzuri.

Ni tuzo ambayo huzingatia zaidi takwimu kama mabao, pasi zinazofika kwa wenzake, pasi muhimu, kufanikiwa kupokonya mipira na kutoruhusu mabao kwa kuangalia nafasi yake uwanjani. Pia huangalia ushiriki wake katika nyakati muhimu zinazobadili mchezo kama kufunga bao muhimu la kuongoza, kuokoa bao la wazi au kuwezesha timu kuondoka katika mazingira magumu.

ZENG 01

Hata hivyo, hayo yote hayawezi kumwezesha mchezaji kuwa MVP hadi timu yake iwe na mafanikio. Na mafanikio hayo huangaliwa yamechangiwa vipi na mchezaji huyo. Ni kwa kiasi gani mchezaji ameinyanyua timu na ustadi wake ukatafsiriwa ndiyo ulioiwezesha timu kushinda na kuondoka na pointi muhimu.

Mchezaji anayeshinda tuzo hii pia huangaliwa ushawishi wake kwa wenzake uwanjani, kiwango chake cha kufanya kazi (work rate) uwanjani, kuwa na nidhamu ya kufuata mbinu za kocha na uwezo wa kuwaongoza na kuhamasisha wachezaji wenzake uwanjani.

Hayo ni lazima yawe yanafanyikwa msimu mzima au sehemu kubwa ya msimu badala ya mchezaji kuibuka kwenye mechi moja au mbili akafanya maajabu na mwishoni apewe tuzo ya MVP.

ZENG 02

Mijadala na ubishi wa nani anastahili kuwa MVP au Mchezaji Bora wa Msimu huchanganya vigezo na hujikita katika takwimu chache binafsi zinazoweza kumsaidia mchezaji kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu, lakini si MVP.

Wengi wanalinganisha takwimu za kufunga mabao na kutoa pasi za mwisho, bila ya kujali mafanikio uya timu yake katika msimu mzima.

Na tuzo hiyo ingetolewa misimu hii mitatu, ukiwemo huu tunaoelekea kuumaliza, kungekuwa na ubishi mkubwa kwa sababu wengi walishajiamulia nani ndiye alistahili kwa kuangalia hizo takwimu chache.

Ulikuwepo msimu uliotawaliwa na mijadala ya ama Pacome Zouzoua na Ahoua, ukawepo pia msimu uliomzungumzia Feisal 'Fei Toto' Salum  na Stephanie Aziz Ki na mjadala ushaanza ukimhusisha Cloutus Chama, Fei Toto na chipukizi Allan Okello na huo pia unahusisha zaidi takwimu za kufunga mabao na kutoa pasi za mwisho na ushiriki katika kufunga mabao (key pass).

ZENG 03

Ni muhimu kwanza dhana ikatengenezwa tunayemtafuta ni Mchezaji Bora wa Msimu au MVP. Na tukishapata dhana tunayotaka ituonmgeze kumpata mchezaji wa aina gani, tutengeneze vigezo vinavyolingana na tuzo na mwishoni tutengeneze mfumo mzuri wa upigaji kura na aina ya wapigakura bila ya kuwaruhusu kukaa vikao vya kujadili wampe nani tuzo; yaani ama kama waandishi wa habari, wachambuzi, manahodha wa timu au makocha ili kusiwe na tuzo za kuridhisha upande fulani kama ilivyozoeleka.