Prime
Aziz KI kurejea Bongo! Matajiri wamfuata
ELIYA SOLOMON
NYOTA wa Al-Ittihad ya Libya, Stephane Aziz KI, ametajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaomvutia kocha wa Azam FC, Florent Ibenge huku taarifa za kurejea kwake Bongo zikishika kasi.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya kiungo huyo kutoka Burkina Faso kuweka wazi kuwa hana pingamizi la kurejea kucheza soka la kulipwa nchini Tanzania endapo masharti yake binafsi ya kimkataba yatafikiwa.
Kwa muda mrefu, Aziz KI amekuwa akihusishwa na kurejea Yanga.
Msimu wa 2023/24, nyota huyo aliandika historia baada ya kufunga mabao 21 katika Ligi Kuu Bara na kuibuka mfungaji bora, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa viungo hatari zaidi.
Ubora wake uliivutia Wydad Casablanca ya Morocco ambayo ilimsajili kwa ada inayokadiriwa kuzidi euro 300,000, zaidi ya Sh917 milioni za Tanzania, kabla ya baadaye kuhamia Al-Ittihad.
Aziz KI aliitumikia Wydad kwa msimu mmoja wa 2025/26, lakini safari yake nchini Libya haijaonekana kuwa na utulivu kama ilivyotarajiwa mwanzoni. Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa kiungo huyo hajawa na furaha katika mazingira yake ya sasa, hali inayochochea uwezekano wa kutafuta changamoto mpya.
Inaelezwa kuwa kurejea Tanzania ni moja ya chaguo analolifikiria kwa uzito kutokana na ukaribu alioujenga na mashabiki pamoja na maisha aliyokuwa akiishi wakati akiwa Yanga. Ndani ya Azam, taarifa zinaeleza kuwa Ibenge amekuwa akivutiwa na uwezo wa Aziz KI tangu akiwa kocha wa Al Hilal ya Sudan ambapo aliwahi kuonyesha nia ya kuhitaji huduma ya kiungo huyo kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi, kufunga mabao na kuiongoza timu.
Iwapo Azam itafanikiwa kumpata, Aziz Ki anaweza kuongeza ubora katika eneo la kiungo mshambuliaji ambalo kwa sasa limekuwa likimtegemea zaidi Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye mabao 14 na asisti nane.