Huyu ndo Artan aliyeondolewa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Msemaji wa FIFA Bryan Swanson amethibitisha katika taarifa yake kwamba Artan amekataliwa kuingia Marekani baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami.
LOS ANGELES, MAREKANI: KWA mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), imesema kuwa mwamuzi wa Somalia, Omar Abdulkadir Artan ameondolewa kuchezesha Fainali za Kombe la Dunia 2026 na shirikisho hilo halina mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi husika.
Msemaji wa FIFA Bryan Swanson amethibitisha katika taarifa yake kwamba Artan amekataliwa kuingia Marekani baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami.
Baada ya mazungumzo na mamlaka za Marekani, FIFA limethibitisha kuwa Artan hatashiriki Kombe la Dunia la mwaka 2026 kama ilivyokuwa imepangwa awali.
"FIFA inaweza kuthibitisha kuwa mwamuzi Omar Abdulkadir Artan hataweza kushiriki mafunzo wala kuchezesha mechi za Kombe la Dunia 2026, baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia Marekani," imesema taarifa ya FIFA.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa FIFA haihusiki na taratibu za uhamiaji za nchi mwenyeji, ikiwamo utoaji wa viza na kwamba mamlaka husika zimeeleza kuwa hali ya Artan haitabadilika kwa sasa.
Mamlaka za uhamiaji za Marekani hazijatoa sababu rasmi ya hatua hiyo, lakini Somalia ni miongoni mwa nchi zilizowekwa kwenye orodha ya marufuku ya usafiri iliyoanzishwa na utawala wa Rais Donald Trump.
Mshauri wa Serikali mjini Mogadishu amesema kwamba Artan ambaye angekuwa Msomali wa kwanza kuwa Mwamuzi katika fainali za Kombe la Dunia alikuwa na visa halali ya kuingia Marekani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi Kazi cha Ikulu ya Marekani kinachosimamia Kombe la Dunia, Andrew Giuliani, ametetea uamuzi huo.
"Siwezi kuzungumzia taarifa za ndani kuhusu suala hilo, lakini naweza kusema ulikuwa uamuzi sahihi wa mamlaka za forodha na ulinzi wa mipaka na ninaunga mkono uamuzi huo," amesema Giuliani.
Artan alikuwa miongoni mwa waamuzi 52 walioteuliwa na FIFA kuchezesha mechi za Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika nchini Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.
Mwamuzi huyo anayetambuliwa na FIFA amewahi kuchezesha mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na anatajwa kuwa mmoja wa waamuzi bora wanaochipukia barani Afrika.
SOMALIA YALALAMIKIA
Maofisa wa Somalia wameitaka dunia ya soka kusimama pamoja kumuunga mkono mwamuzi huyo mahiri baada ya kushindwa kuingia Marekani na hivyo kukosa nafasi ya kuchezesha mechi katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia.
Mshauri mwandamizi wa Wizara ya Vijana na Michezo ya Somalia na nahodha wa zamani wa timu ya taifa, Ciise Aden Abshir, amesemaArtan ni mmoja wa waamuzi wanaoheshimika zaidi barani Afrika na anastahili kuungwa mkono na familia nzima ya soka duniani.
“Omari Artan ni miongoni mwa waamuzi wanaoheshimika zaidi Afrika na anastahili kupata sapoti kutoka kwa jamii nzima ya soka. Kumnyima kibali cha kuingia Marekani na kumzuia kuchezesha mechi alizopangiwa si tu kwamba kunamuathiri binafsi, bali pia kunadhoofisha misingi ya haki, uwezo na roho ya ushindani wa haki katika mchezo wa soka,” amesemaAbshir katika taarifa iliyoripotiwa kwanza na Shirika la Habari la AFP.
ARTAN NI NANI?
Kwa sasa, Artan anaripotiwa kuwa jijini Istanbul, Uturuki, ambako amekuwa akiishi katika miezi ya karibuni. Mwamuzi huyo aliyetajwa kuwa bora zaidi Afrika mwaka jana, alichezesha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2023 na amekuwa mwamuzi wa Shirikisho la Soka la Soka la Kimataifa (FIFA) tangu mwaka 2018.
Artan alikuwa miongoni mwa waamuzi 170, waamuzi wasaidizi na waamuzi wa teknolojia ya VAR waliopangwa kusimamia jumla ya mechi 104 za mashindano hayo yatakayodumu kwa wiki sita. Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, amewahi kumtaja Artan kama “Chanzo cha hamasa kwa kizazi kipya cha Wasomali”.
Changamoto za usafiri na visa zimekuwa zikitajwa kwa muda mrefu kama moja ya hatari zinazoweza kuathiri Kombe la Dunia litakalofanyika Marekani, hasa chini ya sera kali za uhamiaji za utawala wa Rais Donald Trump. Artan ni mmoja wa watu wa karibuni kukumbana na matatizo hayo.
Tayari wachezaji na maofisa wa Iran wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kuingia Marekani kwa miezi kadhaa, hali iliyosababisha kambi yao ya maandalizi kuhamishiwa nchini Mexico.
Wiki hii, maofisa wa Iran walidai baadhi ya watumishi wa benchi la ufundi walinyimwa visa katika dakika za mwisho, madai ambayo yalikanushwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Wakati huohuo, mshambuliaji wa Iraq, Aymen Hussein, alizuiliwa na kuhojiwa kwa takribani saa saba katika Uwanja wa Ndege wa O’Hare jijini Chicago kabla hajaruhusiwa kuingia.
Kiungo wa Uswisi, Breel Embolo, naye alinyimwa visa ya kuingia Marekani wiki iliyopita, lakini mamlaka za Uswisi zilisema zimefanikiwa kukata rufaa na kubatilisha uamuzi huo.