Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ian Wright avunja ukimya Msomalia kuondolewa Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Wright ametoa kauli hiyo baada ya kuibuka kwa taarifa ya mwamuzi wa Somalia, Omar Abdulkadir Artan, kunyimwa ruhusa ya kuingia Marekani licha ya kuwa alikuwa amepangwa kuwa miongoni mwa waamuzi watakaochezesha fainali za Kombe la Dunia 2026.

MAONI makali ya nguli wa soka wa England, Ian Wright, kuhusu sintofahamu zinazoendelea kuelekea Kombe la Dunia 2026 yamezua mjadala mkubwa baada ya kulalamikia kile alichokiita mazingira yasiyo rafiki kwa washiriki wa mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Wright ametoa kauli hiyo baada ya kuibuka kwa taarifa ya mwamuzi wa Somalia, Omar Abdulkadir Artan, kunyimwa ruhusa ya kuingia Marekani licha ya kuwa alikuwa amepangwa kuwa miongoni mwa waamuzi watakaochezesha fainali za Kombe la Dunia 2026.

“Nimesoma tu kwamba mwamuzi wa Somalia amenyimwa kuingia nchini (Marekani). Kila baada ya saa chache ni habari nyingine; mashabiki wananyimwa kuingia, wachezaji wananyimwa kuingia, maofisa wananyimwa kuingia, waandishi wa habari wananyimwa kuingia, sasa hata waamuzi?” amesema Wright akionyesha hasikitiko

Nguli huyo wa zamani wa Arsenal amesema hali hiyo inaibua maswali mengi kuhusu maandalizi ya mashindano hayo, akidai kuwa tiketi za gharama kubwa, malazi yenye bei ya juu na changamoto za usafiri tayari zimekuwa mzigo kwa wengi wanaotarajia kuhudhuria michuano hiyo.

Kauli za Wright zimekuja baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuthibitisha kuwa mwamuzi huyo wa Somalia hataweza kushiriki Kombe la Dunia la 2026 baada ya kukataliwa kuingia Marekani alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami.

Msemaji wa FIFA, Bryan Swanson, amesema baada ya mazungumzo na mamlaka za Marekani, imebainika kuwa FIFA haina mamlaka ya kuingilia maamuzi ya ndani ya nchi husika kuhusu masuala ya uhamiaji na utoaji wa vibali vya kuingia nchini.

Kutokana na hali hiyo, Artan ameondolewa rasmi kwenye orodha ya waamuzi wa Kombe la Dunia 2026, jambo ambalo limeongeza mjadala kuhusu changamoto zinazowakabili baadhi ya washiriki wa mashindano hayo.

Wright amesema anawahurumia mashabiki wa soka wa Marekani ambao walikuwa na matarajio makubwa ya kuona Kombe la Dunia likiwa sherehe ya mchezo huo, akisisitiza kuwa matukio ya aina hiyo yanaweza kuharibu taswira ya mashindano makubwa zaidi duniani.

“Hili ni Kombe la Dunia la sintofahamu. Yeyote atakayeshinda atalazimika kupitia changamoto nyingi sana. Kuna mambo ambayo lazima yazungumzwe,” amesema Wright.

Sakata la Artan sasa limeibua mjadala mpana kuhusu usawa wa upatikanaji wa mashindano hayo kwa washiriki kutoka mataifa mbalimbali, huku wengi wakisubiri kuona kama hatua zaidi zitachukuliwa kuhakikisha Kombe la Dunia 2026 linaendeshwa bila vikwazo vinavyoweza kuathiri washiriki wake.