Anko Kitime: Bendi zetu na muziki wa kuiga
Muktasari:
- Kuna nchi nyingine hufanya mpaka mashindano ya bendi za aina hii ili kuangalia ni kwa ubora gani zimeweza kuiga vizuri. Na mara nyingine inafikia mpaka kunakuwa na mahusiano makubwa ya urafiki kati ya waigaji na wanaoigwa
Dar es Salaam. ‘Cover bands’ ni bendi ambazo hurudia nyimbo za bendi nyingine. Duniani kote kuna ‘cover bands’. Katika nchi nyingine kuna bendi ambazo huiga na kupiga nyimbo za bendi moja tu, na huiga mpaka uvaaji na ‘swaga’ nyingine zote za bendi wanazoziiga.
Kuna nchi nyingine hufanya mpaka mashindano ya bendi za aina hii ili kuangalia ni kwa ubora gani zimeweza kuiga vizuri. Na mara nyingine inafikia mpaka kunakuwa na mahusiano makubwa ya urafiki kati ya waigaji na wanaoigwa.
Hapa kwetu pia bendi za aina hizi zipo nyingi siku hizi, japo kuna tofauti kubwa ya kiutendaji ukilinganisha na bendi nilizozitaja hapo juu. Kwenye miaka ya 60 na 70 na hata kuendelea kidogo, kulikuwa na aina mbili za cover bands hapa nchini.
Kulikuwa na kundi la kwanza ambalo liliiga bendi za Kikongo, lakini katika kuiga huko, waliiga upigaji wa vyombo tu na kutunga maneno ya Kiswahili katika nyimbo hizo. NUTA Jazz Band, Dar es Salaam Jazz Band na Kilwa jazz Band, Western Jazz Band ni kati ya bendi kubwa zilizokuwa na nyimbo nyingi za aina hiyo.
Nyimbo kama Nachekacheka Kilwa Leo, Napenda Nipate Lau Nafasi za Kilwa Jazz Band au wimbo National Service ya NUTA Jazz Band ni mifano mizuri ya uigaji wa nyimbo kutoka Kongo. Lakini bandi hizi zilirekodi nyimbo nyingi ambazo zilikuwa tungo zao halisi.
Kundi la pili la uigaji lilikuwa lile lililokuwa likiiga nyimbo kutoka nchi za magharibi, hata majina ya bendi hizi yalikuwa ya bendi toka huko. Kulikuwa na bendi zilizoitwa, The Sparks, The Comets, The Revolutions, The Flames na kadhalika.
Katika uigaji wa kundi hili wanamuziki walishindana kuiga nyimbo za kizungu kama zilivyopigwa bila kujaribu kubadili chochote, bendi za aina hii zilikuwa maarufu sana kwa wanafunzi wa sekondari, kwani hata wanamuziki wengi wa muziki huu walikuwa wanafunzi, baadaye muziki huu ulikuwa na soko katika mahoteli makubwa nchini.
Kundi hili halikujishughulisha sana na kurekodi nyimbo zao. Siku hizi asilimia kubwa ya bendi hapa nchini zinapiga muziki wa kuiga bendi nyingine, na uigaji wa zama hizi umekuwa mpana zaidi, unahusu kila aina ya muziki. Cover Bands hizi zimejikita kuiga nyimbo za bendi mbalimbali za hapa nyumbani, bendi za zamani zilizokwisha kufa na bendi ambazo bado ziko hai.
Na karibuni cover bands kadhaa zimeanza hata kuiga nyimbo maarufu za muziki wa Bongofleva, Taarab, singeli na hata nyimbo za muziki wa injili. Lakini bahati mbaya idadi kubwa ya bendi hizi hazifanyi mazoezi makini katika kuiga nyimbo hizo hivyo matokeo ni nakala hafifu za muziki ulioigwa, jambo ambalo linashusha thamani ya bendi na hata muziki wa dansi kwa ujumla.
Katika bendi hizi zinazopiga muziki wa kuiga, nyingine hufukia mapungufu yao kwa kujazia vionjo vipya katika nyimbo ambazo wameziiga. Si ajabu kabisa kukuta wimbo kama Georgina wa Safari Trippers au Rangi ya Chungwa wa Nyanyembe Jazz Band, ukiongezwa ‘sebene’ la Wenge Muzika, na kuongezwa vibwagizo vya ‘marapa’ wakihamasisha kwa aina mbalimbali ya maneno, ili japo nyimbo iliyoigwa nusunusu ipate uhai.
Bendi nyingi za zamani huigwa lakini kuna bendi ambazo nyimbo zake nyingi huigwa na kuna bendi ambazo ni nadra sana kusikia nyimbo zake zikiigwa. Kwa hapa nchini kuna bendi kama Urafiki Jazz Band, Biashara Jazz Band na baadhi ya nyimbo za Dar es Salaam Jazz Band.
Upigaji solo wa marehemu Michael Vicent wa Urafiki Jazz Band na upigaji solo wa Marehemu Michael Enoch katika nyimbo zake nyingine za Dar es Salaam Jazz Band, na upigaji wa gitaa wa Juma Ubao wa Biashara Jazz Band, ulikuwa ni wa ufundi mkubwa na ni nadra kuusikia ukiigwa.
Kule Kongo iliwahi kutokea bendi iliyoitwa Orchestra Kiam. Bendi iliyokuwa mali ya Verckys Kiamangwana Mateta na ndio maana iliitwa Kiam kikiwa kifupi cha Kiamangwana. Bendi hii ilikuwa na nyimbo nyingi sana zilizopendwa sana karibu Afrika nzima.
Nyimbo kama Kamiki, Bomoto, Memi, Yangayanga na kadhalika zilitikisa vijana enzi zake. Lakini upigaji wa muziki wa bendi hiyo ulikuwa wa ufundi mkubwa na ulikuwa wa spidi kali kutokana na staili ya muziki wa Kavacha staili iliyokuwa maarufu wakati huo.
Kundi hilo lilikuwa na wanamuziki wazuri sana, waimbaji walikuwa Bakolo Keta, Jeannot Botuli Ilonge, na Frank Muzola Ngunga, wapiga magitaa Lélé Nsundi na Djo Morena, na kwenye gitaa la bezi akiweko Vieux Kody, wakisindikizwa na mpiga drums Suké Ngonge, walikuja na muziki ambao ni nadra kuusikia ukiigwa na hata wale mabingwa wa kunakili.
Kupiga nyimbo za wanamuziki wengine huwa ni njia mojawapo ya wanamuziki kujifunza mambo mpya, wanamuziki wengine hutumia kuiga huku kama ni darasa na hatimaye huweza kuja na kitu kipya kabisa.
Bendi nyingi ambazo ziliwahi kutamba hapa nchini zilitumia njia hii, zilianza kuiga lakini wakati huohuo zikitumia kuiga huko kama darasa, na hatimaye kujitengenezea mtindo wao.
Kwa mfano ukichunguza nyimbo za Vijana Jazz wakati wa mtindo wao wa Koka koka utaona kuwa walikuwa wakifuata nyayo za kundi la Sosoliso la huko Kongo, lakini wakawa wanatunga nyimbo zao na hatimaye kuja na kitu kilichoonekana ni aina ya muziki wa bendi yao.
Hata ukisikiliza nyimbo za Mlimani Park za awali kuna vionjo vinasikika kuwa vilitolewa kwenye bendi ya Verckys. Waliiga wakajifunza wakaja na kitu kipya.
Muda umefika wanamuziki wa muziki wa dansi kujitazama upya kama wanataka kuweka alama katika muziki huo.