Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anko Kitime: Miaka 60 tangu kifo cha Salum Abdallah Yazidu

Muktasari:

  • Ilikuwa kati ya bendi zilizokuwa maarufu sana miaka ya sitini mpaka 70. Nyimbo kama Shemeji shemeji wazima taa, Wanawake, Wangu Ngaiye bado zinapigwa majukwaani na vijana ambao hakika hawakuwahi kuiona bendi hii ikiwa jukwaani.

Dar es Salaam. Cuban Marimba Band ya Morogoro,  ilikuwa ikiongozwa na Salum Abdallah Yazidu.  Bendi ilianza mwaka 1942 ikiitwa La Paloma Band na mwaka 1944 ikabadili jina na kuitwa Cuban Marimba.

Ilikuwa kati ya bendi zilizokuwa maarufu sana miaka ya sitini mpaka 70. Nyimbo kama Shemeji shemeji wazima taa, Wanawake, Wangu Ngaiye bado zinapigwa majukwaani na vijana ambao hakika hawakuwahi kuiona bendi hii ikiwa jukwaani.
 
Alhamisi tarehe 18 Novemba, 1965 ilikuwa siku yenye hekaheka kubwa mjini Morogoro, ugeni mkubwa ulikuwa unasubiriwa katika mji huo.  Mheshimiwa Julius Kambarage Nyerere na Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa, viongozi wakuu wa nchi wakati huo, walikuwa wakisubiriwa na wananchi wa hapa katika sherehe ya  kufungua Chuo cha Kilimo ambacho kwa sasa kinajulikana kama SUA (Sokoine University of Agriculture).

Pamoja na wageni hao pia alitegemewa kuweko aliyekuwa Mbunge wa Morogoro mjini wakati huo Mheshimiwa Oscar Kambona. Bendi mbili kubwa maarufu za pale Morogoro mjini, Cuban Marimba iliyokuwa ikiongozwa na Salum Abdallah na Morogoro Jazz Band zote zilitegemea kupiga siku hiyo, na pia zilipangiwa kutembelewa na viongozi hao wakuu wa nchi.

Kutokana na ushindani mkubwa wa bendi hizo wanamuziki  na mashabiki wa bendi hizo walikuwa roho juu kusubiri mpambano wa usiku huo muhimu katika historia ya mji wa Morogoro. 

Salum Abdallah pamoja na kuwa mwanamuziki maarufu, pia alikuwa na malori ya kubeba mchanga ambayo yalikuwa yakiendelea na kazi kama kawaida siku hiyo, kipindi hicho malori yalikuwa yanabeba mchanga kwa ajili ya mradi wa kujenga nyumba za National Housing pale Morogoro.

Kwenye muda wa saa kumi na mbili jioni baada ya shamrashamra za kupokea viongozi kwisha,  Ramadhan Mdidi aliyekuwa msaidizi wa mmoja wa madereva wa malori ya Salum Abdallah alikuja kumweleza  tajiri wao kuwa, moja ya gari lake limenasa kwenye mchanga katika mkondo wa mto walikokuwa wakichimba mchanga, kwa hiyo ilikuwa busara kuliondoa gari usiku uleule au la kama mvua ingenyesha gari lingeweza kuchukuliwa na maji.

Salum Abdallah akaagiza gari likavutwe.
Salum akamtuma mwanamuziki wake Waziri Nyange atangulie kwenye ukumbi ambako wangepiga muziki ili kutayarisha  vyombo  kwa onyesho la usiku, na yeye akaenda na lori jingine kwenda kuvuta gari lililonasa kwenye mchanga.

Siku hiyo Cuban Marimba walikuwa wapige muziki Community Center wakati wenzao Morogoro Jazz Band walikuwa wapige Kichangani.

Kiasi cha saa moja hivi mmoja wa waliokuwamo kwenye lori lililoondoka na Salum Abdallah alirudi mbio nyumbani na kuwataarifu kuwa kumetokea ajali na Salum ameumia.
 
Ajali hii ilikuwa ya ajabu na kwa miaka mingi ilileta gumzo kwa walioikumbuka. Kwa maelezo ya waliokuwapo, giza lilikuwa limekwisha ingia na wakati lori likikariba Msamvu taa zilizimika ghafla na gari ikayumba lakini taa zikawaka tena, kiasi cha waliokuwemo kuanza kucheka, lakini kicheko chao kilikatika ghafla baada ya kugundua kuwa mlango wa upande aliokuwa amekaa Salum ulikuwa wazi naye amedondoka.

Walirudi nyuma na kumkuta akiwa kalala barabarani akiugulia kwa maumivu. Mzungu mmoja alipita wakati uleule na gari dogo akawapa lifti watu wawili toka kwenye lile lori, mmoja akaenda nyumbani kwa Salum kutoa habari na mwingine akaenda kuchukua taxi iliyomchukua majeruhi mpaka hospitali. 

Hivyo wote waliopata habari wakakimbilia hospitali wakamkuta Salum  anaugulia maumivu, madaktari walimuomba anyooshe mikono na kisha miguu alipoweza, wakaamini hajavunjika bali ni maumivu ya juu juu ambayo yangeisha, kiasi cha kumruhusu arudi kwake na awahi matibabu kesho yake asubuhi. 

Salum mwenyewe akawaambia wenzie wafungue vyombo wasipige  dansi siku ile, wengi wakakesha nae. Usiku kucha ulikuwa wa maumivu makubwa, asubuhi mgonjwa alipelekwa hospitali akafanyiwa upasuaji ikagundulika alivunjika kiuno na mifupa kupasua kibofu cha mkojo, jambo ambalo kutokana na kuchelewa kugundulika lilikuwa ni baya sana.

Kama saa 7 mchana alitolewa chumba cha upasuaji na wenzie waliokuwa wakisubiri wakaambiwa waende makwao wakale vizuri ili waje baadae kutoa damu kwa ajili ya mgonjwa. Wakatoka kwa furaha wakijua mambo yatakuwa mazuri.

 Walielekea kwenye klabu yao wakatengeneza chakula na kula kwa furaha. Kulianza hata kuwa na utani kuwa ,’Mwarabu akipona atatoa kibao cha kikali cha tukio hilo’ Ikumbukwe kuwa baba yake Salum alikuwa Mwarabu halisi, na hivyo rafiki wa Salum walikuwa wakimtania kwa kumuita ‘Mwarabu’.

Lakini ilipotimu saa kumi jioni taarifa ya kusikitisha ikafika kuwa Salum amefariki. Watu wakaanza kumiminika nyumbani kwake, wakakuta hata maiti imeshafikishwa kwake na imewekwa katika chumba kimoja ambacho kilikuwa kimetayarishwa kwa ajili ya frame ya duka.  

Inasemekana baada ya Salum kufariki Daktari Mkuu wa Mkoa aliendesha gari lake hadi nyumbani kwa Salum na kupaki gari lake nje na kuanza kulia jambo ambalo mara moja ndugu walielewa kuwa mambo yameharibika, hivyo waliweza kutayarisha  sehemu hiyo ambayo iliwezesha watu kuja kuweza kuona mwili wa Salum kwa mara ya mwisho.

Haikuchukua muda habari zilisambaa na ulinzi ukalazimika ukimarisha kwa kusaidiwa na polisi kutokana na wingi wa watu waliofika. Watu wakakesha na marehemu .

Kesho yake hali ilizidi kuwa ngumu wakati wa kusindikiza maiti kwenda makaburini ilikuwa kama kila mtu alikuwa akitaka japo aguse kidogo jeneza, hadi ikalazimu FFU wawepo kuleta amani. Jeneza la Salum liliweza kubebwa kutoka Nunge nyumbani kwa mama yake hadi Msamvu kwenye eneo alipozikwa, watu wakiwa wamejipanga mstari mrefu, hakukutumiwa gari.

Wimbo wake huu alioutunga muda mfupi kabla hajafa ulileta tafsiri nyingi hasa kutokana na kifo chake cha ajabu
E Mola wangu E Mola wangu,
Nivue na ya dunia,
Hao walimwengu, hao walimwengu ,
 Wanitafuta kwa madawa,
Wataka wadhulumu roho yangu,
Wapate furahiwa,
Natoa salamu zangu,
Ningalimo mu dunia,
Kwa ndugu na jamaa zangu
Za mapenzi na furaha
Za kuwatoa uchungu
Ajali itakaponifikia
Nahadithi ndugu zangu,
Nyuma waliobakia,
Kibeba maiti yangu
Huku wakinililia
Nitamshtakia Mungu
Nilotendwa mu dunia

MOLA AMLAZE PEMA SALUM
YAZIDU ABDALLAH