Hatima ya kanisa la Mc Pilipili, baada ya kuonekana sehemu za starehe

Muktasari:

  • Kutokana na tetesi za kuvunjika kwa ndoa yake na kuonekana maeneo ya starehe kulipelekea baadhi ya watu kudai kuwa kwa sasa waumini wote wameondoka katika kanisa hilo na kusababisha Pilipili alifunge kabisa kwani hakuna watu wa kusali.

Licha ya kuwa anafanya vizuri kwenye upande wa uchekeshaji na u-MC lakini pia Pilipili ni mchungaji, awali alikuwa na kanisa lililoitwa Love Church, maeneo ya Mwenge, Dar es Salaam .

Kutokana na tetesi za kuvunjika kwa ndoa yake na kuonekana maeneo ya starehe kulipelekea baadhi ya watu kudai kuwa kwa sasa waumini wote wameondoka katika kanisa hilo na kusababisha Pilipili alifunge kabisa kwani hakuna watu wa kusali.

Pililipili anaiambia Mwananchi Digital kuwa hadi sasa ni mwaka tangu afunge kanisa lake ambalo alikuwa anakodisha ukumbi na kukutana na waumini wake kwa ajili ya ibada, sababu ya kufanya hivyo anasema ni kuweka mambo sawa kwa ajili ya kuwafikia zaidi waumini wake na siyo vinginevyo.

“Muda mrefu kama mwaka hatukutani kwenye ibada tunaweka vizuri mambo halafu tutarudi tena, siyo kama nimesimama kabisa kutoa huduma, kama nitakuwa na kanisa nitaongea na watu hamsini Mungu yeye anataka niongee na watu wengi zaidi kwa hiyo huduma itarudi tena, napanua watu wa kuwafikia, ambao siyo lazima mtu aje kanisani anaweze kusikia neno la Mungu hata akiwa anaendesha gari,” alisema.

Hofu ya kupoteza waumini wake wa mwanzo baada ya kuacha kutoa huduma Pilipili amesema, hilo halimpi shida kwa sababu hata mwanzo hakuwa na watu bali walikuja wenyewe kupata huduma.

“Nilikuwa na watu kama mia mbili wengine wapo Marekani watu ni wa Mungu sina wasiwasi wa kuwapoteza. Kwanza kwa sasa hatutafungua kanisa ila itakuwa ni huduma ya Mungu ambayo itahudumia watu wa makanisa yote litaitwa Kingdom Of God”. alisema.

Safari ya Pilipili hadi kuwa mchungaji

Pilipili anasema ameokoka tangu mwaka 1994, akiwa darasa la nne, Dodoma.
“Nilibaatizwa kwa maji mengi na nikaendelea kusali nilipofika kidato cha kwanza nilianza kuwa mwalimu wa watoto kanisani kwa miaka mitano, baadaye nikawa mchungaji wa vijana na kisha nikawa msaidazi wa mchungaji, kilichikuwa kinazuia nisiwe mchungaji kamili sikuwa nimeoa kipindi hicho.

Nilivyokuwa kidato cha kwanza nilikuwa kiongozi wa Ukwata humo ndipo nimehubiri sana nilifikia hatua ya kujaza watu kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma nikamleta Rose Muhando, Fanuel  Sedekia na Upendo Kilahiro ”. Anasema

Anasema alivunja rekodi ya somo la dini kwa Dodoma  akapata nafasi ya kwenda kusimamia shule za kanisa kama mwalimu wa masomo ya dini.

“ Mimi unavyosikia mwalimu siyo wa hesabu au Civics ni wa masomo ya biblia kwa madarasa ya mitihani kuanzia form two , four na six hata ukimsikia Mon Centrozone anasema mimi mwalimu wake ni kwenye masomo ya dini hayo Civics nilianza kufundisha baadaye,”alisema.

Kutokana na hayo Pilipili anakanusha maneno ya baadhi ya watu wanaodai aliingia kwenye huduma ya uchungaji mara baada ya kifo cha mama yake, anasema yeye siyo mtu ambaye amekurupuka kwenye dini, anaijua tangu utotoni na hata mambo mengine anayofanya yanafanikiwa kutokana na kuokoka kwake.

Kwa sasa ana Stashahada ya Uchungaji na anaendelea na masomo, anachukua Shahada ya uchungaji kwenye Chuo Cha Biblia kilichopo Kawe kiitwacho Shalom Bible College.


Pilipili kuzunguka na mchanga kwenye chupa Dar nzima

Mchekeshaji huyu anaeleza kwa mara ya kwanza alipofika Dar es Salaam alienda Kawe na kuchota mchanga wa eneo hilo na kuuweka kwenye chupa, kisha kuzunguka nao Dar nzima akiwa amefunga ili aweze kuiteka Dar.

“Nilienda kwenye mkutano wa Ukwata wa Taifa Moshi neno likasema mimi ni nuru ya ulimwengu, ndiyo nikajua kumbe ninaweza kuwa sehemu yoyote nchini au duniani na 'nikashaini', nilivyokuja Dar kabla mtu yeyote hajanijua nilichukua mchanga wa kawe kwenye chupa  nikazunguka nao nikiwa nimefunga kwa wiki moja nikimuomba Mungu anipe Dar  lakini akanipa Taifa nzima na ndiyo maana Tanzania hakuna Mc aliyenifikia mimi.

Pilipili anaonekana sehemu za kula bata

Mbali na hayo Januari 18, Pilipili aliwashangaza wengi baada ya kuonekana kwenye sehemu ya starehe akiwa na msanii Diamond, Haji Manara na mkewe Zaylissa, kitendo hicho kilipelekea baadhi  ya watu kukosoa kumuona kwake sehemu hiyo kwa sababu wengi wanamfahamu kama mchungaji.

Pilipili amesema kwa upande wake hatumii kilevi chochote kwa hiyo watu kabla ya kuongea kuwepo kwake sehemu hiyo ilitakiwa wamuulize kwa nini ameenda, kwa sababu  lengo baya la kitu huwa kwenye kusudio.

“Element imekuwepo miaka mingi mimi sijawahi kuonekana pale, nilionekana baada ya kualikwa na Haji Manara,  Zaylissa mimi ni shabiki wake, nilialikwa baada ya wao kuvalishana pete ya uchumba kulikuwa na ‘afta pati’.

Ndivyo ilivyotokea, mimi ile sehemu haijanivuta ni Haji Manara na hata angesema anataka kwenda katikati ya bahari au Morogoro ningeenda, Haji alisema anaenda Element sasa mimi ningekataaje?”.  Anasema mchekeshaji huyu.

Anasema washikaji wote ni wake kwa hiyo ataendelea kukaa nao, watu wengi wataendelea kumuona kwenye sehemu hizo kwa sababu hata kwenye maandiko ya vitabu vya dini yanasema  nuru haitakiwi kuogopa giza