Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Marioo, Paula ni uhusiano wa faida kazini

Muktasari:

  • Ikiwa ni takribani miaka miwili tangu wawe pamoja na miezi sita baada ya kujaliwa mtoto wao wa kwanza Princess Amarah, Paula, binti wa Kajala Masanja na P-Funk Majani anaonekana kugeuka lulu katika kazi ya Marioo.

Dar es Salaam, Ndivyo tunavyoweza kusema kufuatia staa wa Bongo Fleva kutokea Bad Nation, Marioo kuendelea kumtumia mpenzi wake na mzazi mwenzie, Paula katika video za nyimbo zake ambazo sasa zimefikia tano.

Ikiwa ni takribani miaka miwili tangu wawe pamoja na miezi sita baada ya kujaliwa mtoto wao wa kwanza Princess Amarah, Paula, binti wa Kajala Masanja na P-Funk Majani anaonekana kugeuka lulu katika kazi ya Marioo.

Nyota ya Marioo kimuziki ilianza kung’aa baada ya kuurudia wimbo wa Lameck Ditto, Moyo Sukuma Damu (2016) ambao ulimvutia Prodyuza Emma The Boy na kumuomba Ruge Mutahaba ampe nafasi pale Tanzania House of Talent (THT).

Mwaka mmoja baadaye alikuja kutoka na ngoma yake, Dar Kugumu (2018) iliyotayarishwa na Abbah, kwa sasa ana utitiri wa nyimbo zilizofanya vizuri hadi kushinda Tuzo Tano za Muziki Tanzania (TMA) huku akiwa ametoa albamu moja, The Kid You Know (2022).

Kitendo cha Marioo kuanzisha uhusiano na Paula, binti aliyekulia katika mazingira ya kishua na familia ya watu maarufu, kinatoa maana kamili ya neno ‘kupambana’ kwa sababu bila hivyo pengine ingekuwa vigumu kwa yeye kuwa naye.

Kufanya kazi gereji hadi leo hii kuwa miongoni mwa wanamuziki wanaofanya vizuri na wenye ushawishi Tanzania, ni wazi Marioo amepambana sana lakini kuwa na Paula kunazidi kumuongezea nguvu katika kazi yake ya sanaa.

Ni hivi karibuni Paula ameonekana mwanzo hadi mwisho katika video ya wimbo mpya wa Marioo, Unachekesha (2024) ambayo inafanya vizuri kwa sasa ikishika nafasi za juu chati za YouTube katika nchi mbalimbali.

Hii inakuwa video ya kwanza kwa wawili hao kufanya pamoja tangu wamejaliwa mtoto ila ya tano baada ya Lonely (2023), Tomorrow (2023), Sing (2023) na Hakuna Matata (2024) iliyotoka kipindi Paula ni mjamzito.

Paula ni staa mwingine Bongo kufanya video katika hali hiyo (ujauzito) baada ya Nandy katika wimbo wake ‘Napona’ kutoka katika EP yake ya tatu, Maturity (2022), huku mumewe Billnass akitokea pia katika video hiyo aliyoshirikishwa Oxlade wa Nigeria.

Tangu ametoka kimuziki miaka sita iliyopita, Marioo amefanya video na warembo mbalimbali ila Paula ndiye pekee aliyemtumia kwa zaidi ya mara moja na ni wazi amefanya hivyo kwa sababu ni mpenzi wake.

Ikumbukwe kwa mara ya kwanza Paula kuonekana katika video ya muziki ilikuwa katika ile ya Rayvanny, Wanaweweseka (2021) ambayo ilitoka kipindi akiwa na uhusiano na mwimbaji huyo kutokea Next Level Music (NLM).

Na sasa Marioo na Paula wanapita njia ya Rayvanny na mpenzi wake na mzazi mwenzie Fahyma ambaye wamefanya video sita pamoja ambazo ni Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023), Habibi (2023) na Mwambieni (2023).

Diamond Platnumz kutokea WCB Wasafi ni msanii mwingine Bongo ambaye amefanya kama Marioo na Rayvanny, waliowahi kuwa wapenzi wake na sasa wamebaki kama wazazi wenza, Zari The Bosslady na Hamisa Mobetto walitokeo katika video zake.

Zari kama alivyojaliwa watoto wawili na Diamond, Tiffah (2015) Nillan (2016), yeye ametokea video mbili za nyimbo za Diamond, Utanipenda (2015) na Iyena (2018) na ndiye mpenzi pekee wa Diamond aliyefanya naye video nyingi.

Kwa upande wake Hamisa, Miss XXL After School Bash (2010) ambaye uhusiano wake na Diamond ulikuwa wa siri sana hadi walipojaliwa mtoto, Dylan (2017), aliinogesha vizuri video ya Diamond, Salome (2016) akimshirikisha Rayvanny.

Ukiachana na kuwapa nafasi katika video zake, pia Diamond amewahi kutoa wimbo pamoja na video na aliyekuwa mpenzi na mzazi mwenzie ambaye ni Tanasha Donna, Mwanamitindo na Mtangazaji wa zamani wa NRG Radio Kenya.

Wawili hao walishirikiana katika wimbo ‘Gere’ kutoka katika EP yake ya kwanza Tanasha, DonnaTella (2020) iliyotoka ikiwa na nyimbo nne na kuwapa shavu wasanii wengine kama Mbosso na Khaligraph Jones.

Tanasha ni mpenzi wa pili wa Diamond aliyepata nafasi ya kurekodi wimbo pamoja na mwanamuziki huyo baada ya Hamisa ambaye alisikika katika wimbo, Jibebe (2018) uliowakutanisha Mbosso na Lava Lava pia ingawa hakutajwa kama ameshiriki katika wimbo huo.