Mwana FA aliimbia Mabinti, nao wamemuheshimisha!

Muktasari:

  • Mabinti unawekwa kundi moja na nyimbo kama ‘Mamsapu’ wa Hard Blasters Crew (HBC), ‘Hayakuwa Mapenzi’ wa Mr. II Sugu, ‘Zali la Mentali’ wa Professor Jay, ‘Chochote Popote’ wa Joh Makini

Dar es Salaam, Moja ya nyimbo zilizopo katika albamu ya kwanza ya Mwana FA, Mwanafalsafani (2002) ni ‘Mabinti’ ambao hadi sasa unatajwa kuwa miongoni mwa nyimbo kali za mapenzi upande wa Hip hop kuwahi kutokea Bongo.

Mabinti unawekwa kundi moja na nyimbo kama ‘Mamsapu’ wa Hard Blasters Crew (HBC), ‘Hayakuwa Mapenzi’ wa Mr. II Sugu, ‘Zali la Mentali’ wa Professor Jay, ‘Chochote Popote’ wa Joh Makini n.k.

Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa miaka zaidi ya 20 katika muziki alitoa albamu mbili, Mwanafalsafani (2002), Toleo Lijalo (2003) na albamu moja ya ushirikiano, Habari Ndio Hiyo (2008) akiwa na AY.

Ikumbukwe Februari 2, 2002 ndio siku ya kwanza kwa wimbo wa kwanza wa Mwana FA kusikika redioni, wimbo huo ‘Ingekuwa Vipi’ alimshirikisha Jay Moe na ulirekodiwa Mawingu Studio na Bonny Luv ambaye alimsubiri kwa miezi 18 arudi kutoka Uingereza.

Ikiwa ni miaka 20 tangu wimbo wa ‘Mabinti’ umetoka, jina la wimbo huo hadi sasa lina maana kubwa katika muziki wa Mwana FA, kwa hakika mabinti wana mchango sana kwa kumpa namba kubwa  katika mtandao wa YouTube.

Hivi unajua kuwa video za Mwana FA ambazo zimetazamwa zaidi YouTube kwa muda wote, zote nyimbo zake amewashirikisha mabinti, yaani wasanii wa kike ambao ni Vanessa Mdee (Dume Suruali), Maua Sama (Gwiji) na Linah (Yalaiti)?.  

Mosi, Dume Suruali (2016) akimshirikisha Vanessa Mdee, ndio wimbo namba moja wa Mwana FA kutazamwa zaidi YouTube ukiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 6.6.

Wimbo huo uliotengenezwa na Daxo Chali pale MJ Records na kupewa jina la ‘Sitoi Hela’ kabla ya ‘Dume Suruali’, ni miongoni mwa nyimbo ambazo aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli alieleza kuvutiwa nazo .

Pili, Gwiji (2020) ni wimbo aliyowashirikisha Maua Sama na Nyoshi El Saadat, huku ukitengenezwa na Mr. T Touch, video yake tayari ina ‘views’ zaidi ya milioni 2.3 ndani ya miaka yake mitatu.

Utakumbuka Mwana FA ndiye alimtoa Maua Sama kimuziki baada ya kukubali kushiriki katika wimbo wake, So Crazy (2013) na baadaye kumsimamia kimuziki kabla ya kujiunga na Tanzania House of Talent(THT).

Tatu, Yalaiti (2014) akimshirikisha Linah, wimbo huu una ‘views’ zaidi ya milioni 2.0, Mwana FA aliwahi kusema kwake wimbo huu ni mkali kuliko ‘Mabinti’ linapokuja suala la nyimbo kali za Hip hop upande wa mapenzi.

Ikumbukwe Mwana FA alianza kujifunza muziki kupitia kundi la Quite Gangsters Chronic (QGC) Dar es Salaam, alipoenda Tanga  kusoma akajiunga na kundi la Black Skin. Na jina la Mwanafalsafa (Mwana FA) alipewa na Bonny Luv.