Nancy Sumari afichua siri alivyoshinda Umiss Tanzania

Muktasari:
- Nancy amesema hayo siku moja baada ya kifo cha baba yake huyo mzazi kilichotokea jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
Dar es Salaam, Miss Tanzania mwaka 2005, Nancy Sumari amesema kuwa baba yake Edward Sumari (71) alimpa sapoti kubwa katika kuyafikia mafanikio hayo.
Nancy amesema hayo siku moja baada ya kifo cha baba yake huyo mzazi kilichotokea jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Sikumfurahisha kwa sababu alitamani kuona nasoma kwa sababu alikuwa anapambana kuwekeza kwetu kutokana na akili za ujana niliamua kushiriki na nakumbuka nilikuwa natakiwa kwenda chuo mwaka wa kwanza,” anasema na kuongeza;
“Nashukuru Mungu nilifanya nilichokuwa natamani kufanya na Mungu alikuwa upande wangu nikafanya vizuri na nikarudi chuo pia nilifanya vizuri baba yangu alifurahi sana.”
“Hakuwa msomi lakini alipambana na kufanikiwa kiuchumi kwa mapambano yake lakini hakutamani kuona familia yake inapita njia zake ametuacha akiwa ametutengenezea maisha kwa kupambana kuhakikisha tunapata elimu bora.”
Anasema licha ya baba yake kuwekeza kwao ili wasome lakini pia alikubali katika ndoto za wanae watano na mwingine mmoja ambaye alimlea.
Akizungumzia kifo cha baba yake, Nancy alisema kimetokea muda mfupi baada ya kumaliza kuabudu.
“Muda mchache kabla ya baba kufariki Dunia tulizungumza akatufahamisha kuwa anasali na sisi pia tulikuwa tunamuombea lakini tukiwa tunaendelea na ibada tulipata taarifa ya umauti wake,” alisema na kuongeza;
“Kauli yake ya mwisho alituambia kuwa anatupenda na sisi tulimwambia tunampenda pia tunamshukuru Mungu kwa ajili yake tunajivunia kwa kuwa alikuwa baba bora kwetu siyo bora tu alikuwa ni nyumba nzima maana kuna wengine wanasema nguzo ya familia sisi wetu alikuwa zaidi,” amesema Miss Tanzania huyo wa zamani.
Mzee Sumari atazikwa Jumatano huko nyumbani kwake Mererani, Arusha